March 31, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

GST yaongeza makusanyo kwa asilimia 91 serikali ya awamu ya sita

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania(GST)katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita imeongeza makusanyo ya ndani kutoka wastani wa shilingi 1,251,428,472.91 mwaka 2021 hadi shilingi 2,394,211,348 mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 91.32.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 27,2025 na Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST Nokta Banteze wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.

Pia Banteze amesema idadi ya sampuli zinazochunguzwa imeongezeka kutoka wastani wa sampuli 19,184 mwaka 2021 hadi sampuli 25,793 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 34.45. 

Vilevile bajeti ya taasisi hiyo imeongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 10 mwaka 2021/2022 hadi bilioni 110 mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 1,000 kwa ajili ya kukamilisha majukumu mbalimbali ya taasisi ikiwemo miradi ya maendeleo.

“GST ilikamilisha ugani wa jiolojia kwa lengo la kubaini miamba na madini yanayopatikana kwenye QDS 278 na 290 zilizopo Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere na Pori la Akiba la Selous – katika sehemu ya Mikoa wa Lindi na Ruvuma); QDS mbili mpya  ambazo ni QDS 203 na 204 katika sehemu ya Mkoa wa Pwani na sehemu ndogo ya Mkoa wa Dar es salaam.

“Matokeo ya awali ya utafiti  yameonesha uwepo wa mchanga wa ujenzi, madini ya dhahabu na urani kwenye QDS 278 na 290 na uwepo wa madini ya kaolin, chokaa, udongo mfinyanzi, silica sand, madini tembo na metali adimu kwenye QDS 203 na 204,”amesema Batenze.

Aidha Banteze amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita,imefanikiwa kufanya mageuzi mbalimbali katika nyanja ya utafiti , upimaji wa sampuli za madini na  utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini.

Ambapo amesema GST imekamilisha mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini 2733
yaliyohusu uchukuaji wa sampuli wakilishi na utambuzi wa jiolojia ya maeneo yenye uwepo wa madini katika mikoa ya Lindi,Morogoro,Geita na Mwanza.

“GST imefanikiwa kufanya utafiti wa madini ya helium  katika mikoa ya Arusha , Manyara, Dodoma, Singida na Shinyanga na kubaini kiwango cha helium katika chemchem za majimoto zinazofaa kwa hatua ya utafiti wa kina katika maeneo ya Ziwa Natron na Eyasi,”amesema.

Akizungumzia mwelekeo wa GST Banteze amesema Serikali kupitia GST katika mwaka 2025/2926 kuwa,imepanga kufanya utafiti wa kina kw kutumia ndege ili kuongeza asilimia  za utafiti wa kina kutoka asilimia 16 mpaka 34 , ikiwa na lengo la kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Vilevile imepanga kujenga maabara ya kisasa (state of art labaoratory) katika mkoa wa Dodoma kwa ajili kuimarisha uchunguzi wa  sampuli za madini nchini ili kuchochea shughuli za utafiti nchini na hivyo kuhamasisha ukuaji wa Sekta ya Madini. Maabara husika itakuwa na vifaa vya kisasa na itaweza kufanya uchunguzi wa sampuli za madini nyingi zaidi ikiwemo zinazojumuisha madini muhimu na kimkakati.

“GST imepanga kujenga majengo ya kisasa ya maabara na Ofisi katika mikoa ya Geita na Mbeya ili kuwasogezea huduma karibu zaidi wachimbaji madini ikiwemo wachimbaji wadogo wa madini. Kukamilika kwa ujenzi huo kutaongeza tija kwa wachimbaji wa madini kwa kuwapunguzia kuchimba kwa kubahatisha.

Pamoja na hayo Banteze amesema GST imekusudia kukamilisha ujenzi wa mfumo wa usimamizi wa taarifa na takwimu za Taifa za madini. Kukamilika kwa mfumo huo utaongeza ufanisi katika utunzaji na usambazaji wa taarifa za madini na hivyo kuchochea uwekezaji katika sekta ya madini.