Na Mwandishi Wetu, Timesmajira
TIMU ya soka ya GSM FC, imemtambulisha rasmi aliyekuwa kocha wa zamani wa Kagera Sugar na Ndanda FC Mussa Mbaya maarufu kama ‘Moloto’, kwa ajili ya kuifundisha timu hiyo katika mashindano ya Kombe la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kocha huyo alitambulishwa rasmi leo, mbele ya waandishi wa habari kwenye makao makuu ya GSM, Salamander Tower mtaa wa Somora jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia kuhusu timu hiyo, Mtendaji Mkuu wa GSM FC Ali Kamwe amesema walikuwa na orodha ya makocha wengi lakini walihitaji kocha mwenye kiwango cha hali ya juu na kufanikiwa kumpata Moloto.
Mbali na hilo, amesema timu hiyo imefanya uwekezaji mkubwa ili iweze kunyakuwa Kombe la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ndio maana wameajili kocha wa kiwango.
“Hii ndiyo timu ya tajiri Ghalib Said Mohammed (GSM), kule Yanga SC yeye ni mfadhili tu, lakini hii ndiyo timu yake, ndiyo maana tunasema tunakwenda kuchukua ubingwa wa mashindano haya kwakuwa tuna uwekezaji mkubwa.
“Hii ndiyo timu pekee yenye wadhamini wawili kwenye mashindano ya Ramadhan Cup, wadhamini hao ni Haiertanzania na Maxfashion,” alisema Ali Kamwe.
Naye Meneja wa timu hiyo, Kibwana Matokeo alisema kutokana na kuwa na benchi la ufundi zuri wanaamini watafanya vizuri kwenye mashindano hayo.
“Tuna benchi kubwa la ufundi ndiyo maana tunajiamini kwa kusema tutafanya vizuri kwenye mashindano haya ya Ramadhan Cup,” alisema Kibwana Matokeo.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania