- Awahimiza wataalamu kusimamia zoezi la kuziunganisha Gridi za Tanzania na Kenya kwa umakini bila kuathiri upatikanaji wa umeme kwenye mfumo wa Gridi ya umeme Nchini
- Aeleza faida za Tanzania kufanya biashara katika soko la EAPP na SAPP
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) Mha. Gissima Nyamo-Hanga amesema kuimarika kwa mfumo wa Gridi za Umeme za Tanzania na Kenya kutasaidia kuimarisha upatikanaji wa umeme katika ukanda wa Kaskazini Mashariki mwa Afrika .
Mha.Gissima ameyasema hayo Desemba 20,2024 wakati wa Ziara yake akiongozana na Viongozi wengine wa Shirika katika kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme cha Lemuguru kilichopo Mkoani Arusha.
“Niwahimize wataalamu mnaosimamia mfumo wa Gridi mnapoendelea na zoezi la kuunganisha mifumo ya Gridi za Tanzania na Kenya kuhakikisha zoezi hilo haliathiri upatikanaji wa umeme kwenye Mfumo wa Gridi yetu nchini “. Alisisitiza Mha Gissima.
Mha. Gissima amesema kituo hicho cha Lemuguru ni muhimu kutokana na kuunganisha mfumo wa Gridi ya Taifa na mifumo mingine ya Gridi ya nchi za ukanda wa Kaskazini Mashariki mwa Afrika( EAPP ).
Muunganiko huu kikanda wa Eastern African Power pool una jumla ya Nchi wanachama 13.
Mbali ya muunganiko wa Gridi ya umeme ya Tanzania na upande wa Kaskazini mashariki mwa Afrika, Mha.Gissima amesema Tanzania inaendelea na Mradi utakaounganisha Gridi yetu na mifumo ya Gridi zingine za nchi zilizo Kusini mwa Afrika yaani Southern African Power Pool.
Akielezea faida zitakazopatikana kutokana na Tanzania kushiriki soko la Kikanda la biashara ya umeme kwa kuingia katika muunganiko wa kuuziana na kununua umeme kwa ukanda wa Kaskazini Mashariki (EAPP) na ukanda wa Kusini mwa Afrika (SAPP), Mha. Gissima amesema nchi itafaidika kwa kuuza umeme kutokana na uwekezaji mkubwa Serikali inaoufanya katika miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme nchini.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara ya Kikazi ya Menejimenti ya Shirika kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ambapo walianzia katika mradi wa kimkakati wa kufua umeme kwa nguvu ya maji wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best