Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
KAMPUNI ya Greatlakes Freight & Transport imewapiga tafu waogeleaji wa Tanzania wanaowania nafasi ya kufuzu mashindano ya Olimpiki yaliyopangwa kufanyika mjini Tokyo, Japan kuanzia Julai 23 hadi Agosti 8, 2021.
Waogeleaji hao wawili, Collins Saliboko na Hilal Hilal walichagulia na Chama cha kuogelea Tanzania (TSA) kusaka tiketi ya kufuzu mashindano ya Olimpiki yaliyopangwa kufanyika Mei 7 na 8 mjini Stellenbosch, Afrika Kusini.
Wakati Collins akidhaminiwa kuanzia mazoezi ya Gym na kwenye maji, Hilal ambaye alikuwa mazoezini Dubai, amedhaminiwa tiketi ya kwenda Afrika Kusini ambapo ndipo yatakapofanyika mashindano hayo na iwapo watafuzu, waogeleaji hao watashiriki mashindano hayo ya Olimpiki.
Mkurugenzi Mkuu wa Greatlakes Freight & Transport, Fahmy Ahmed amesema, wameamua kusaidia waogeleaji hao pamoja na mchezo wa kuogelea ili kuleta hamasa na maendeleo kwa vijana.
Fahmy amesema kuwa, udhamini wao kwa waogeleaji hao ni kama sehemu ya kampuni kujihusisha na shughuli za kijamii, kuendeleza vipaji vya vijana wa leo na kuhamasisha mchezo huo na kuyataka makampuni mengine kuwaunga mkono vijana hao ili waweze kupeperusha vema bendera ya Tanzania bila vikwazo na mawazo yanayoweza sababishwa na upungufu wa mazoezi na vifaa stahiki.
Amesema, mchezo wa kuogelea una vipaji vingi nchini pia ni mchezo ambao unatazamwa zaidi katika mashindano ya Olimpiki lakini kwa hapa nchini, mchezo huo unashindwa kuendelea kutokana na kukosa sapoti kutoka kwa jamii na hasa udhamini.
“Makampuni mengi yanapendelea zaidi kudhamini michezo maarufu, kama mpira wa miguu na ngumi na kuona mchezo wa kuogelea hauna tija na wala haufahamiki. Nawashauri watu kuweka bidii kwenye mchezo huu kwa kuwa una waogeleaji wengi ambao wanaweza kuitangaza nchi nje ya mipaka yake,” amesema Fahmy.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TSA, Asmah Hilal ameipongeza kampuni hiyo kwa msaada mkubwa na kuwawezesha waogeleaji hao kujiandaa na kwenda kushindana kuwania nafasi ya kufuzu Olimpiki.
Lakini pia aliishukuru Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na dula la kuuza vifaa vya michezo la Just Fit kwa kusaidia waogeleaji hao ambao walikuwa njia panda kwenda kushiriki katika mashindano hayo ambayo ni muhimu kwa ajili ya kutafuta nafasi ya kufuzu Olimpiki.
“Kwa niaba ya TSA, napenda kutoa shukrani kwa kampuni ya Greatlakes Freight & Transport kuweza kusaidia waogeleaji wetu. Kwa kweli tulikuwa njia panda na ujio wao dakika za mwisho umesaidia kufanikisha safari yao,” amesema Asmah.
Waogeleaji hao wameongozana na kocha Alex Mwaipasi ambapo watapata mafunzo na mwenyekiti wa kamati ya ufundi ya Shirikisho la mchezo huo duniani (FINA), Graham Hill kabla ya mashindano rasmi.
Pia yupo muogeleaji chipukizi, Austin Okore kutoka klabu ya Dar Swim ambaye atahudhuria mafunzo ya kunoa kipaji chake ambayo yamedhaminiwa na Shirikisho la mchezo huo Barani Afrika (CANA) ambao wanalipia gharama za kulala, chakula na masuala mengine muhimu kwa kila muogeleaji.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania