Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online
KOCHA mkuu wa klabu ya Simba, Didier Gomes Da Rosa ameweka wazi kuwa timu yao ipo tayari kupambana na wenyeji wa mchezo wao Kaizer Chiefs katika mchezo wao wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Mei 15 kwenye uwanja wa FNB.
Simba itaingia katika mchezo huo huku ikitaka kuendeleza rekodi bora waliyoiweka katika hatua ya Makundi ambapo walifanikiwa kumaliza kileleni mwa Kundi A baada ya kufikisha alama 13 walizopata baada ya kushinda mechi nne, sare moja na kupoteza mechi yao ya mwisho dhidi ya Al Ahly.
Simba pia walifanikiwa kuweka wavuni goli tisa na kuruhusu goli mbili pekee moja katika ushindi wa goli 4-1 dhidi ya AS Vita na nyingine ni katika mchezo dhidi ya Ahly uliomalizika kwa goli 1-0.
Licha ya rekodi hiyo katika Ligi Mabingwa lakini Simba wameendelea kuwa bora ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) baada ya kushinda mechi tano mfululizo wakiwafunga Mtibwa goli 5-0, Mwadui 1-0, Kagera Sugar 2-0, Gwambina 1-0 na Dodoma Jiji 3-1.
Rekodi hizo ni tofauti na zile za wapinzani wao walioshinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza mechi moja lakini wakifunga goli tano na kuruhusu goli sita huku katika Ligi yao ya ndani wakipoteza mechi tatu dhidi ya Cape Town City, Chippa United na Tshakhuma, wakitoka sare na Bloem Celtic na Baroka FC na kushinda goli 2-1 dhidi ya vinara wa Ligi hiyo, Mamelodi Sundowns.
Kocha huyo amesema kuwa, wapo tayari kwa ajili ya kucheza mchezo huo ambao wameusubiri kwa muda mrefu.
Amesema, kwa hakika wanatambua kuwa mchezo huo utakuwa mgumu lakini watahakikisha wanacheza kwa kujitoa na morali ya ushindi kwani wanachokitaka ni kuwapa furaha Watanzania na mashabiki wa Simba.
Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu amesema kuwa wanaondoka na wachezaji 24 na leo kiungo Benard Morrison ataungana na wenzake kwa ajili maandalizi ya mwisho kuelekea kwenye mchezo huo muhimu.
Kama timu wamejiandaa kupata ushindi lakini wakitambua hakuna mchezo rahisi kutokana na uhitaji wa ushindi kwa kila mmoja hivyo jambo kubwa ni kumuheshimu mpinzani wao ambaye naye ni bora hasa anapokuwa nyumbani kwake.
Akizungumzia mchezo huo, Nahodha wa Simba, John Bocco amesema kuwa wanatambua kuwa watakwenda kukutana na ugumu mkubwa katika mchezo huo kwani wanaelewa kuwa wapinzani wao ni wazuri na wana uzoufu na mashindano hayo.
Amesema kitu pekee kitakachowasaidia kupata ushindi katika michuano hiyo ni maandalizi waliyoyafanya na watakayoyafanya kwa siku zilizobaki na wanaamini katika kupata matokeo mazuri.
“Kaizer Chiefs ni timu nzuri, kubwa na yenye uzoefu na mashindano haya, tunajua kuwa tutakutana na changamoto zitakazofanya mchezo kuwa mgumu lakini sisi tunaamini maandalizi yetu ndiyo yatakayotupa matokeo mazuri katika mchezo huu,” amesema Bocco.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania