Gharama Kubwa za Tiba Magonjwa Makubwa Zatajwa Bungeni
Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma
CHANGAMOTO ya gharama kubwa za matibabu kwa magonjwa sugu kama figo, selimundu, saratani, kusafisha damu na moyo imekuwa ikiwakumba wananchi na hivyo baadhi yao kupoteza maisha.
Akizungumza Juni 2,2025 Bungeni jijini Dodoma wakati wa mjadala kuhusu bajeti ya Wizara ya Afya iliyowasilishwa na Waziri wa Wizara hiyo ya sh.1.6 Trilioni,Mbunge wa Moshi Vijijini  Profesa Patrick Ndakidemi aliiomba serikali kuongeza juhudi za kutoa ruzuku kwa matibabu ya magonjwa hayo, ili wananchi wa kawaida wasiendelee kuteseka au kupoteza maisha kutokana na kukosa uwezo wa kugharamia tiba.
Aidha , Profesa Ndakidemi aliipongeza serikali kwa kuwekeza kiasi cha shilingi bilioni 4 katika jengo la mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ingawa hata hivyo, aliongeza kuwa bado yapo majengo mengine katika hospitali hiyo ambayo yanahitaji uboreshaji na kuomba serikali iendelee kuwekeza hapo kwani KCMC ina wataalamu wabobezi wanaotoa huduma za hali ya juu ikiwemo upasuaji wa nyonga, mfumo wa chakula, tezi dume, tiba ya ugumba na utengenezaji wa viungo bandia.
Katika kuonyesha mchango wa hospitali hiyo kwa jamii, Profesa Ndakidemi alisifu hatua ya KCMC kutoa msamaha wa matibabu kwa wagonjwa 4,002 ambapo jumla ya shilingi bilioni 2.1 zilitumika kusaidia wananchi hao kupata tiba bure. Alisema huo ni mfano wa kuigwa na hospitali nyingine nchini, na ni uthibitisho kuwa sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali pia zina nafasi kubwa katika kuboresha afya ya jamii.
Kuhusu maendeleo ya huduma za afya katika jimbo lake, Profesa Ndakidemi alikumbusha ombi la mashine ya kidijitali ya E-RAY kwa Hospitali ya Kibosho ambalo aliiomba kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024, na kuomba lizingatiwe tena mwaka huu.
Aidha, aliomba serikali itoe vifaa tiba na magari kwa vituo vya afya vya Uru Kusini, Uru Shimbwe, Kibosho Umbwe, pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Mabogini ili huduma ziboreshwe zaidi kwa manufaa ya wananchi wa Jimbo Hilo na Taifa kwa ujumla
Profesa Ndakidemi pia aliitaka serikali kutatua changamoto mbalimbali za huduma za tiba ambazo bado zinawakabili wananchi wengi.
Alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa dawa, vifaa tiba kama vitanda, majokofu ya kuhifadhia dawa na maiti, magari ya wagonjwa, na chanjo hasa maeneo ya vijijini ambako huduma bado ni duni. Alisema hakuna sababu ya watu kupoteza maisha kwa matatizo yanayoweza kuzuilika iwapo serikali itawekeza ipasavyo.
Kuhusu ugonjwa wa selimundu, aliangazia takwimu kutoka kwa hotuba ya Waziri Mhagama kuwa asilimia 15 ya Watanzania wana vinasaba vya selimundu na tayari watu 34,000 wamegundulika kuwa na ugonjwa huo. Kati yao, ni watu 11 pekee waliofanyiwa upandikizaji wa uroto sawa na asilimia 0.03, hali inayoonyesha ukosefu wa rasilimali za kutosha kwa ajili ya tiba hiyo. Alisema serikali haina budi kuweka mkakati wa kutoa ruzuku ili tiba hizo zipatikane kwa wengi zaidi.
Aidha ,Profesa Ndakidemi alieleza masikitiko yake kuhusu idadi ndogo ya wananchi walioko kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Alisema gharama kubwa za bima hiyo zimekuwa kikwazo kwa Watanzania wengi kujiunga, jambo linalopelekea watu wengi kutoenda hospitali hata wanapougua.
Alisema serikali inapaswa kupitia upya viwango vya mchango wa bima hiyo na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga ili afya bora iwe ya wote, si ya wachache wenye uwezo.
More Stories
Yas yaja na ‘Anzia Ulipo’ kuhamasisha watanzania kusimamia ndoto zao
Coca-Cola Kwanza kuwanufaisha mama lishe Stendi ya Msamvu Marogoro
Sheikh Ponda akabidhiwa kadi ya heshima ya Maalim Seif