December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya wafanyakazi wa GGML wakizungumza na wageni wanaotembelea banda la kampuni hiyo ilililopo katika maonesho ya teknolojia ya madini mjini Geita jana. Na mpiga picha wetu.

GGML mdhamini mkuu maonesho ya teknolojia za uchimbaji madini

Na Mwandishi Wetu,timesmajira,online Geita

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imekuwa mdhamini mkuu wa Maonyesho ya Tatu ya Teknolojia za uchimbaji madini mkoani Geita yaliyoanza jana yakitarajiwa kumalizika Septemba 27, mwaka huu.

Kampuni ya GGML imetoa udhamini wa kiasi kinachozidi sh. milioni 200 za zikihusisha gharama za kusawazisha eneo la maonesho pamoja na kugharamia mabanda 100 na umeme wa dharura (jenereta na mafuta yake) katika kipindi chote cha maonesho hayo.

Maonyesho hayo ambayo yanafanyika katika viwanja vya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji na Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) Mjini Geita ambalo pia limejengwa na Kampuni ya GGML kupitia mpango wake wa huduma kwa jamii kwa gharama za sh. milioni 800.

“GGML inajivunia kudhamini maonesho haya kwa mwaka wa tatu mfululizo. Mwaka huu tunakusudia kutoa uzoefu wetu wa matumizi ya vifaa mbalimbali vya uchimbaji kwa makampuni mengine lakini pia kwa wachimbaji wadogo.

Ni jambo zuri pia kwamba tumetoa udhamini huu tukiwa tunaadhimisha miaka 20 ya uwekezaji wetu mkoani Geita na Tanzania. Tunajivunia kuendeleza ushirikiano na jamii inayotuzunguka kunufaisha wafanyabiashara wa ndani wanaokusudia kufanya kazi na sisi,” alisema Makamu wa Rais wa GGML, Simon Shayo anayeshughulikia miradi endelevu.

Alisema wanafarijika sana kuona ndoto ya kuwa na kituo cha Uwekezaji na biashara ya nje hapa Geita inatimia na GGML inakuwa sehemu ya mafanikio hayo kupitia mpango wake wa kusaidia jamii.

“Pamoja na tunu yake kuu ya kuisaidia jamii ya Geita kuwa na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi ambayo yatabakia hata baada ya shughuli za uchimbaji kumalizika, Kampuni ya GGML pia imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Geita ikiwemo uwekezaji wa mradi wa Kituo cha Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji na Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) Mjini Geita uliotumia bajeti ya sh. milioni 800 za Kitanzania.

Maonyesho haya yatakutanisha kampuni za uchimbaji madini, wachimbaji wadogo na wa kati, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na nchi nyingine kwa ajili ya kuonesha teknolojia zinazotumika katika sekta ya uchimbaji madini na fursa za uwekezaji na biashara kwenye sekta hiyo.