Ok okNa Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MKURUGENZI wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel, ameishukuru China kwa kufungua mipaka yake huku akiuomba Ubalozi wan nchi hiyo nchini hapa kufungua dirisha maalum kwa wanafunzi wanaoomba visa kwenda kusoma nchini humo.
Mollel amesema kuna idadi kubwa ya wanafunzi wa Tanzania ambao wangependa kwenda kusoma nchini China hivyo ameuomba Ubalozi wa nchi hiyo nchini kufungua dirisha hilo ili wanafunzi wanaoomba Visa wapate kwa haraka na kwa wakati.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya kuwaaga vijana 46 wa Tanzania wanaokwenda kusoma fani mbalimbali nchini China kwa ufadhili wa serikali ya nchi hiyo kupitia fursa ambayo hutolewa kila mwaka.
Mollel amesema kwa miaka mitatu mfululizo China ilikuwa imefunga mipaka yake hivyo wanafunzi kushindwa kwenda nchini humo lakini anashukuru kwamba hali imerejea kama kawaida na wanafunzi wa Tanzania wameanza kwenda nchini humo.Amesema wanafunzi wanapaswa kuripoti vyuoni mwezi Septemba hivyo aliomba ubalozi huo kuwapa upendeleo wa Visa za haraka haraka wanafunzi wanaokwenda kusoma nchini humo.
“Tuwape fursa wanafunzi kufanya online booking mapema kwasababu tarehe 15 Septemba wanatakiwa kuripoti vyuni kwa hiyo wanatakiwa kupata kabla ya muda huo sasa tukiwacheleweshea wanaogopa kuomba vyuo vya China,” amesema na kuongeza kuwa
“Lakini Booking ndiyo inachukua muda mrefu nawaomba mfungue dirisha maalum kwa wanafunzi wanapoomba Visa wawe wanapata kwa urahisi na kwa haraka tukiweza kufanya hili tutakuwa tumewamasisha wanafunzi wetu wengi kwenda kusoma China,” amesema Mollel.
Amesema kutokana na uhusiano mwema uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na China, GEL itaendelea kushirikiana na serikali ya nchi hiyo kuhamasisha wanafunzi wengi wa Tanzania kwenda kusoma kwenye vyuo mbalimbali vya nchini humo.
Mollel amesema China ina vyuo vingi bora ambavyo vinatoza gharama za kawaida kumuwezesha kila Mtanzania anayetaka kwenda kusoma nchini humo kumudu gharama hizo za masomo.
“Kama mwanafunzi anataka kusoma vyuo vyenye mchanganyiko wa tamaduni, mahudhurio makubwa ya wahadhiri, usalama wa kutosha na gharama ndogo basi China ni chaguo bora kwa sababu haya yote yapo,” amesema Mollel.
“Kwa hiyo wakati wowote serikali inapofikiria kuwapeleka wanafunzi nje ya nchi hata kupitia mpango wa ufadhili wa bodi ya mikopo, bajeti ile ile mnayowapa wanafunzi kwa vyuo vya Tanzania inaweza kukidhi gharama za vyuo vya China,” amesema.
More Stories
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano