January 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gekul apangua tuhuma katiba za TFF na TOC

Na Doreen Aloyce, TimesMajira Online, Dodoma

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul ameweka wazi kuwa, si Shirikisho la Soka nchini (TFF) wala Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ambao wamewahi kubadili Katiba za vyama vyao kwa lengo la kuwalinda viongozi walioko madarakani.

Gekul ametoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Makunduchi, Ravia Idarus Faina ambaye pia aliwahi kuwa rais wa Chama cha Soka visiwani Zanzibar (ZFA), ambaye alihoji ni kwanini vyama hivyo vimekua vikibadili Katiba zao kwa lengo la kulinda viongozi walipo madarakani na kudhibiti Watanzania wengine wasigombee katika vyama hivyo.

Amesema, jambo hilo si kweli kwani vyama hivyo vinasajiliwa kwa sheria ya Baraza la Michezo (BMT) namba 12, 1967 na marekebisho namba 6 ya 1971 na yale namba 3, 2018 pamoja na Kanuni za Msajili za mwaka 1999.

Pamoja na mahitaji ya kubadili Katiba za Vyama kujitokeza na kufanyika, Katiba hizo haziwezi kuanza kufanya kazi mpaka zisajiliwe upya na Msajili wa Vyama ambaye hupitia upya kuona kama kanuni zinazosimamia michezo na sheria nyingine zinaendana na Sheria nyingine za nchi.

Ikiwa msajili ataona swala lililoingizwa katika katiba halina maslahi kwa chama na Taifa ikiwemo masuala ya Utawala Bora, msajili amepewa mamlaka kisheria kukataa usajili huo kwa mujibu wa kanuni za usajili za 1999 (11:3 a, b).

“Napenda kulialifu Bunge lako kuwa, TFF wa la TOC hawajawahi kubadili katiba zao kwa ajili ya kuwalinda viongozi waliopo madarakani kwani mabadiliko hayo yote ya kikatiba ni lazima yakidhi vigezo vya usajili vinavyosimamiwa na Msajili ikiwemo Utawala Bora na ukomo wa muda wa uongozi,”.

Kuhusu TOC, Gekuli amesema kuwa, kwa sasa wanaendelea na marekebisho ya Katiba yao ambayo ilirekebishwa 2019 na 2020 msajili aliipitisha Novemba na katika marekebisho wameweka ukomo wa kiongozi ni mihula mitatu.

“Wamekubaliana kiongozi atakayeingia madarakani basi adumu kwa vipindi vitatu ambavyo ni saw ana miaka 12 na baada yah apo agombee nafasi za juu zaidi hivyo wameboresha vipengele vyote ambavyo vilionekana kuminya uhuru wa watu wengine kugombe,” Amesema Naibu wazuri huyo.

Akijibu swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum, Sofia Mwakagenda lililohoji juu ya uwepo wa ubabaishaji katika mchezo wa ngumi hasa katika nafasi ya urais na je? Serikali haoni haja ya kusimamiao viongozi hao wanaokaa madarakani muda mrefu bila kufuata Katiba, Gekul amesema kuwa, kupitia kwa BMT na Msajili wataendelea kufuatilia jambo hilo na katiba zote zilizochomeka vipengele vya aina hilo.

“Jambo hili tumelipokea na wakati tunaendelea kulifuatilia pia nitafanya ziara katika maeneo hayo na kupitia katiba yao upya tuone ni wapi wameviweka hivyo nawahakikishia kupitia Msajili tunalishughulikia lakini pia wadau wa ngumi watoe ushauri wao pale wanapoona katiba hizo zinakandamiza uhuru wa wadau wengine wenye nia za kugombea,” amesema Gekul.