Na Grace Kisyombe, Geita
MKOA wa Geita na maeneo ya jirani yameanza kunufaika na mradi mkubwa wa umeme wa Geita-Bulyanhulu baada ya kukamilika rasmi kwa mradi huo wenye laini ya kusafirisha umeme mkubwa katika msongo wa Kilovolti 220 sambamba na vituo viwili vya kupoza na kusambaza umeme.
Akifanya ziara na kushuhudia uwashwaji umeme kwa mara ya kwanza katika mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel, amesema kuwa, kwa muda mrefu Mkoa wa Geita ulikuwa na umeme usio tosheleza mahitaji.
“Hali iliyopelekea Serikali kufanya jitihada za kujenga mradi huu Mkubwa ulio gharimu zaidi ya shilingi Bilioni 50 ili kuwezesha wananchi wa Mkoa wa Geita na maeneo ya jirani kupata umeme wa uhakika na gharama nafuu” amesema Mhandisi Gabriel.
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha Geita hivi sasa kumewezesha Mkoa wa Geita kuwa na umeme wa uhakika utakaowezesha uwekezaji katika sekta mbali mbali hususan uchimbaji wa Madini na Viwanda.
Mhandisi Gabriel aliwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika Mkoa wa Geita baada ya ujio wa Umeme wa uhakika na gharama nafuu wa TANESCO.
“Hali sasa ni shwari , umeme upo wa kutosha na wa uhakika. kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha Geita kumewezesha mkoa kuwa na zaidi ya Megawati 85 wakati matumizi ya sasa ya ni Megawati 16 pekee” ameongeza Mhandisi Gabriel.
Aidha, Mhandisi Gabriel amewaasa wananchi wa Mkoa wa Geita na maeneo ya jirani ambapo miundombinu ya umeme imepita kuilinda miundombinu hiyo kwa manufaa ya kizazi hiki na kizazi kijacho.
Mhandisi Gabriel pia ametoa onyo kuhusu tabia ya wananchi kuchoma moto mashamba kiholela, hali inayohatarisha miundombinu ya umeme.
Ameongeza kuwa kwa mwananchi yoyote atakaye bainika kufanya uharibifu huo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ili iwe fundisho kwa wote wenye nia za namna hiyo.
Kwa upande wa TANESCO, Mhandisi Emanuel Manirabona ambaye ni Meneja Mwandamizi wa Miradi -TANESCO amesema kuwa mradi huo wa ujenzi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme ni miongoni mwa miradi mikubwa ya umeme inayojengwa katika kanda ya ziwa na kanda ya magharibi kaskazini mwa Nchi.
Mhandisi Manirabona ameitaja miradi hiyo kuwa ni njia ya umeme ya Geita-Nyakanazi yenye uwezo wa Kilovolti 220, utakao gharimu zaidi ya shilingi Bilioni 100 pamoja na ule wa Kigoma hadi Nyakanazi msongo wa Kilovolti 400.
“yote hii ni kuhakikisha kuwa maeneo ya Uwekezaji katika kanda ya ziwa na kanda ya magharibi kaskazini mwa Nchi yanapata umeme wa uhakika na wakutosha” Alisema Mhandisi Manirabona.
Manirabona aliongeza kuwa, kuungwa kwa njia ya kusafirisha umeme ya Bulyanhulu-Geita, kunawezesha wananchi wa mkoa wa Geita na Maeneo ya jirani na Migodi ya Bulyanhulu pamoja na Geita kuwa na umeme wa uhakika.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi