Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Karatu
NYOTA wa riadha kutoka klabu ya Talent ya jijini Arusha, Gabriel Geay na Failuna Matanga wameng’ara katika Tamasha la Michezo la Karatu (KSF), baada ya kuibuka washindi kwa upande wa wanaume na wanawake.
Tamasha hilo la 19 la Michezo na Utamaduni la Karatu lilifanyika mjini Karatu, mwishoni mwa wiki kwa kushirikisha michezo mbalimbali ikiwamo Riadha, Wavu, Soka, Mbio za Baiskeli, Kwaya na Ngoma za Asili.
Geay ambaye tangu awali alionesha nia ya kumaliza wa kwanza baada ya muda mrefu kuwa mbele, alimaliza mbio hizo za kilometa 10 akitumia dakika 30:47:87 na kuwashinda wakali wengine kama Fabian Nelson wa Polisi alimaliza nafasi ya pili baada ya kutumia dakika 30:58:19, Mathayo Sombi wa Talent akimaliza nafasi ya tatu akitumia dakika 31:02:16 na Inyasi Sulle naye wa Talent alimaliza wa nne kwa muda wa 31:03:84.
Geay amefanikiwa kutetea ubingwa wake alioutwaa mwaka jana na hivyo kuendelea kutamba katika mbio hizo, ambazo hufanyika kila mwaka.
Kwa upande wa wanawake, katika mbio za kilometa tano licha ya kuanguka na kuchubuka miguuni na mikononi, Failuna Matanga ambaye ni kati ya wanariadha waliofuzu kwa Olimpiki Tokyo 2020, alitamba baada ya kuibuka wa kwanza kwa kutumia dakika 17:43:20 huku akifuatiwa na Anastazia Dolomongo wa Maranatha aliyetumia dakika 17:54:20 na Catherine Range wa Magereza aliyetumia dakika 18:06:61 huku mwanariadha mzoefu Jackline Sakilu wa JWTZ akimaliza wa nne dakika 18:15:85.
Failuna amesema kuwa, mbio hizo zilikuwa na changamoto nyingi ikiwemo barabara moja kuwa katika ujenzi na kuifanya kuwa finyu na kusababisha wanariadha kupita kwa tabu sana.
Akielezea kuanguka kwake, Failuna amesema kuwa, mkimbiaji mwenzake mmoja alikuwa akimkanyaga mara kwa mara, na kusababisha kuanguka na kuchubuka vibaya miguuni na mikononi.
Amesema, kama angekuwa mwanariadha mwingine angeanguka kama yeye, asingeweza kuendelea na mbio hizo kwani yeye aliendelea kukimbia huku akiwa na maumivu makali, lakini alivumilia.
Kwa upande wa mchezo wa baiskeli, Masunga Nduba wa Simiyu, alifanya kweli baada ya kuibuka mshindi wa kwanza na kuwapita wakali wa Arusha waliokuwa wakitumia baiskeli za kimashindano pale alipomaliza wa kwanza kwa kutumia saa 1:39:06.36 wakati mshindi wa pili alikuwa Dudubaya Chanjagila wa Sengerema aliyetumia saa 1:39:58:71.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi ambaye ndiye muandaaji wa tamasha hilo amesema, tangu waanze tamasha hilo miaka 19 iliyopita wamekuwa wakitoa zawadi za fedha taslimu pamoja na vifaa vya michezo.
Bayi amesema kuwa, tatizo kubwa la Karatu ni uvamizi wa viwanja vya michezo kugeuzwa maeneo ya kilimo na ujenzi wa nyumba, jambo mbalo limefanya watoto na vijana kukosa maeneo ya kuchezea.
Tamasha hilo la Karatu lilifungwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Iddi Kimanta, aliyetoa zawadi kwa baadhi ya washindi huku akiwapongeza waandaaji ambao ni Taasisi ya Filbert Bayi kwa kuandaa tamasha zuri lililoshirikisha michezo mbalimbali.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania