March 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gawio kutoka kampuni ambazo Serikali ina hisa chache zapaa kwa asilimia 236

Na Penina Malundo, Timesmajira

Gawio kwa Serikali kutoka kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache limeongezeka kwa asilimia 236 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Katika mwaka ulioishia Juni 2024, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina ilipokea kiasi cha Sh195 bilioni kama gawio, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh58 bilioni miaka mitano nyuma.

Hayo yalisemwa Jumatano, Machi 19, 2025, na Lightness Mauki, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) anayesimamia Utendaji, Ufuatiliaji na Tathimini-Mashirika ya Kibiashara.

Mauki alikuwa anazungumza katika kipindi cha Baragumu kinachorushwa na kituo kimoja wapo cha Televisheni nchini, kuelekea Mkutano wa Maafisa Watendaji Wakuu na Wakurugenzi wa Bodi za Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache unaotarajiwa kuanza Machi 26 hadi 28, 2025.

“Huu sio ukuaji wa kawaida,” alisema Bi. Mauki wakati wa kipindi kinachorushwa kuanzia saa 1 hadi 2 asubuhi.

Amesema ongezeka la gawio lilichagizwa na mazingira mazuri ya biashara, kuimarika kwa utawala bora na ushirikiano mzuri na wanahisa wengine.

Pia, ameongeza, ili kuongeza mchango wa kampuni ambazo Serikali ina Hisa chache, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea kupitia mikataba iliyopitwa na wakati ili iendani na wakati wa sasa.

“Kitu kizuri ni kwamba tumeendelea kuwa na mahusiano mazuri na wanahisa wenzetu. Hii itasaidia kuongeza tija ya kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache”

“Ni katika muktadha huo, tumefanikiwa kuongeza umiliki wa hisa zetu katika kampuni ya Madini ya SOTTA kutoka asilimia 16 hadi kufikia asilimia 20,”amesema

Pia,amesema Serikali imeendelea kuboresha utendaji kazi wa kampuni hizo na tayari matunda yake yameanza kuonekana.

Mwezi Juni 2024, Kampuni ya Saruji ‘Mbeya Cement Company Limited’ ilitangaza malipo ya gawio la Sh3 bilioni kwa Serikali ikiwa ni miaka 10 tangu malipo ya mwisho yafanyike.

Amesema lengo la Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kuona Serikali inapata mara mbili ya Sh195 bilioni kama gawio kwa siku za usoni.

Ili hili liwezekane, Ofisi hiyo imeona haja ya kufanya Mkutano wa pili wa Maafisa Watendaji Wakuu na Wakurugenzi wa Bodi za Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.

Katika mkutano huo unaotarajiwa kufanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha, Pwani, utafanyika uzinduzi wa Muongozo wa Utendaji wa wakurugenzi wa bodi unaokidhi malengo tofauti na ule wa awali.

Katika mkutano huo, miongoni mwa mada zitakazowasilishwa ni namna ya kutumia teknolojia katika utendaji wa taasisi ili kuongeza tija na Utawala bora.

Mauki ameamini matumizi ya teknolojia yatakuwa na matokeo chanya kwa utendaji wa taasisi na ndio maana wameamua iwe dhima ya mkutano.

“Serikali ina mahitaji mengi sana. Ni kazi yetu kuhakikisha tunakuja na mbinu mbalimbali katika kupata pesa. Ni muhimu kuongeza makusanya ya gawio ili tuelekeze fedha kwenye miradi ya maendeleo,” amesema Mauki.

” Tunaamini tutaweza kuongeza makusanyo kwani takwimu ziko upande wetu. Kwa kipindi cha miaka minne iliyopita gawio kutoka kwa kampuni ambazo Serikali ina hisa chache limekuwa likikuwa kwa wastani wa asilimia 50 kwa kila mwaka.”

Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya taasisi 308, huku 252 zikiwa ni zile ambazo Serikali ina umiliki wa asilimia 100 na 56 ni zile za umiliki wa hisa chache.