December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gavana wa Fedha asema ,dola ipo ya kutosha mwaka mzima

Na David John ,Geita

GAVANA wa Benki Kuu (BoT) Emmanuel Tutuba amesema amesema,moja ya majukumu ya Benki hiyo ni pamoja na kushiriki katika masuala ya uchumi ambapo hununua dhahabu kwa ajili ya kutunza akiba za nchi badala ya kutunza kama fedha.

Tutuba ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la BoT kwenye maonyesho ya Madini mkoani Geita kwenye viwanja vya EPZA kata ya Bombambili.

Amesema lengo la kununua dhahabu kuziuza nje ya nchi na kupata fedha za kigeni na hivyo kuwezesha kusapoti uchumi wa nchi.

“Kwa hiyo ushiriki wetu katika masuala ya kiuchumi ni pamoja na kununua dhahabu ikiwa ni namna mbadala ya kuendelea kutunza akiba za nchi badala ya kutunza kama fedha taslimu lakini pia tunanunua dhahabu ili tupate fedha za kigeni baada ya kuuza nje na fedha ziweze kusapoti uchumi wa nchi.”amesema Tutuba 

Akizungumzia kuhusu kuadimika kwa dola Tutuba amesema,changamoto hiyo ni kutokana na kuadimika kwa dola  kwenye mzungu wa uchumi kidunia .

Hata hivyo amesema,pamoja na changamoto hiyo BoT bado ina dola za kutosha kugharamia shughuli za kiserikali pamoja na shughuli za kipaumbele  kwa wakati huo.

“Hii ni kutokana na ‘reserves’ ya Dola ilitunzwa na BoT,lakini sasa watu wengine wanachanganya, wakisikia reserves za nchi wanadhani ni fedha ambayo ya kuwagawia watu ,lakini kimsingi hizi reserves ndio zinasaidia nchi katika kipindi kama hiki ambacho dola imeadimika.”amesisitiza Tutuba na kuongeza kuwa 

“Kwa hapa tunaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa serikali kwa kuwa tunayo fedha ya kutosha kutekeleza miradi malimbali kwa mwaka mzima..,lakini hata pakitokea hatari na mipaka ikifungwa zile fedha tunaweza kuzitumia kwa mwaka mzima.”

Gavana Tutuba ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa Filamu yake ya Royal Tour ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza Dola kutokana na watalii wengi kuja kutalii hapa nchini.

“Kwa hiyo katika mzunguko kitakwimu dola inaendelea  kuongezeka na hivyo kuondoa kikwazo cha kuzuia uchumi uendelee.”

Akizungumza kuhusu uwepo wao katika maonesho hayo amesema,wameshiriki kikamilifu kwa lengo la  kutoa elimu kwa wadau wanaohitaji kujua namna BoT  inavyoshiriki kwenye sekta ya madini.

Aidha amesema ,BoT ina dhamana ya kusimamia masuala ya ukuaji wa uchumi na uhimilivu wa bei pamoja na mzunguko  na thamani ya fedha .

“Sisi tumefika katika maonesho haya ikiwa ni mojawapo ya mikakati yetu ya kutoa elimu kwa wadau wa madini na wananchi kwa ujumla kuhusu BoT na kushiriki katika masuala ya ukuaji wa uchumi.”amesisitiza Gavana huyo