December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gavana BoT aanika uamuzi Kamati MPC kupandisha riba

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) imepandisha Riba ya Benki Kuu (CBR)
kutoka asilimia 5.5 iliyotumika katika
robo ya kwanza ya mwaka 2024 hadi
asilimia sita, ambayo itatumika katika
robo ya pili ya mwaka 2024.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana
na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), Emmanuel Tutuba, wakati
akizungumza kwenye mkutano wa
viongozi wa benki na waandishi wa
habari.

Alifafanua kwamba uamuzi wa
kuongeza riba ulifikiwa katika kikao cha
kamati kilichofanyika juzi Aprili 3, 2024
na umezingatia tathimini ya mwelekeo
wa uchumi iliyofanyika Machi 2024.

“Kamati imeona umuhimu wa
kuongeza riba ya Benki Kuu hadi
asilimia sita, itakayokuwa na wigo wa
asilimia mbili juu na chini, ili kukabiliana
na ongezeko la mfumuko wa bei siku
zijazo kutokana na athari za mwenendo
wa uchumi wa dunia” alisema.

Alisema benki zenye ukwasi mdogo
zitapata fedha hadi kwa asilimia nne.
Gavana Tutuba alisema katika robo ya
kwanza ya mwaka 2024, mfumuko wa
bei umeendelea kupungua, sambamba
na kuimarika kwa ukwasi katika masoko
ya fedha na bei za bidhaa katika soko
la dunia imebaki tulivu.

“Mathalani, bei ya mafuta ghafi
ilikuwa wastani wa Dola 80 za Marekani
kwa pipa, wakati bei ya dhahabu
imeendelea kubaki juu, ikiuzwa kwa
wastani wa Dola 2,071 kwa wakia
moja. Hali hii inatarajiwa kuendelea
katika kipindi kijacho cha mwaka 2024”
alisema.

Hata hivyo, alisema matarajio hayo
yanaweza kuathiriwa na uamuzi
wa nchi zinazozalisha mafuta kwa
wingi (OPEC+) kuhusu kiwango cha
uzalishaji na migogoro ya kisiasa
inayoendelea.

Gavana Tutuba alisema akiba ya
fedha za kigeni imeendelea kuwa ya
kutosha, kufikia zaidi ya Dola 5.3 bilioni
mwishoni mwa Machi 2024, sawa na
miezi 4.4 ya uagizaji wa bidhaa na
huduma nje ya nchi.

Aliongeza kwamba nakisi ya urari
wa biashara nje ya nchi iliendelea
kupungua kutokana na kupungua kwa
gharama za uagizaji wa bidhaa na
kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi.

Katika mwaka unaoishia Februari
2024, nakisi ilipungua kufikia Dola
milioni 2,701.4 kutoka Dola milioni
5,133.6 katika kipindi kama hicho
mwaka 2023. Kuhusu thamani ya
Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani.

Alisema ilipungua kwa asilimia 1.8
katika robo ya kwanza ya mwaka 2024
ikilinganishwa na asilimia 1.6 katika
robo ya mwisho ya mwaka 2023.

Hali hii ilitokana na msimu wa
mapato madogo ya fedha za kigeni na
mazingira ya kiuchumi duniani.

“ Kamati pia ilijadili kuhusu
changamoto ya upungufu wa fedha za
kigeni nchini na kujiridhisha kwamba,
hatua za kuongeza upatikanaji na
kupunguza matumizi ya fedha za kigeni
zinazotekelezwa hivi sasa zinatarajiwa
kupunguza changamoto hiyo ndani ya
muda mfupi ujao” alisema.

Kuhusu hatua hiyo, Mwenyekiti wa
Chama cha Mabenki Tanzania (TBA),
Theobald Sabi ameishukuru BoT kwa
usimamizi wa sekta ya fedha nchini,
akiomba suala la uhaba wa Dola
liendelee kushughulikiwa.

“Taarifa ya uamuzi wa riba imetolea vizuri, lakini kuendelea kufanyia kazi suala la uhaba wa fedha za kigeni ni jambo la muhimu.

Sera ya fedha inasimamiwa vizuri
tutakuwa na maoni katika majukwaa
yetu mengine,” alisisitiza Sabi.