January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sehemu ya maeneo yaliyoathirika kwa vurugu, Somalia

Gavana anusurika kufa Putland

PUTLAND, Gavana wa Jimbo la Puntland lenye utawala wake wa ndani nchini Somalia amejeruhiwa vibaya kufuatia mashambulizi ya kujitoa muhanga dhidi yake, ambayo kundi la kigaidi la al-Shabaab linasema limehusika nayo.

Mashambulizi hayo dhidi ya Gavana Abdisalan Hassan Hersi wa Mkoa wa Nugaal yalitokea juzi katika mji mkuu wa Puntland, Garowe.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa jimbo hilo, Mohamed Abdirahman, kamanda wa zamani wa polisi na raia mmoja nao pia walijeruhiwa kwenye mashambulizi hayo.

Mashahidi walisema,mshambuliaji alijilipua mbele ya gari waliyokuwemo gavana huyo na wenzake.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lilifukuzwa kutoka mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, tangu mwaka 2011, na tangu hapo limepoteza ngome zake nyingi, lakini bado linadhibiti maeneo makubwa nje ya Mogadishu.

Pia kundi hilo lenye mafungamano na al-Qaida linapigania kuiondowa serikali inayoungwa mkono kimataifa, likiwa limeshafanya mashambulizi kadhaa mjini Mogadishu.