Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online, Tanga
JESHI la Polisi Mkoa Tanga linamshikilia, Simon Tarimo (37) Mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kusafirisha kilo 133 za mirungi kwenye jokofu linalotumika kuhifadhia jeneza wakati wa kusafirisha maiti.
Mirungi hiyo ilikuwa ikisafirishwa kutoka Usangi kwenda jijini Dar es Salaam kwa kutumia gari maalum zinazotumika kusafirisha maiti.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tanga jana, Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga, Blasius Chatanda amesema mtuhumiwa huyo ambaye ni dereva alikamatwa saa mbili za usiku katika kijiji cha Manga Kata ya Mkata tarafa ya Mazingara wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Kamanda Chatanda amesema mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa na mirungi bunda 1,685 akiwa amezihifadhi kwenye mifuko 6 ya Sulfate akitumia gari ndogo namba T569 DSZ aina ya Volvo ambalo ni maalumu kwa ajili ya kubebea maiti.
Aidha kamanda Chatanda amesema gari hilo ni mali ya kampuni ya Nuru Funeral Service iliyopo jijini Dar es Salam ambalo utumika kusafirisha maiti.
“Mbinu iliyotumika ni kuweka mifuko kwenye jokofu linalotumika kuhifadhia jeneza lenye maiti wakati wa kusafirisha, kitendo ambacho ni kinyume cha matumizi ya gari hilo,” “amesema Kamanda Chatanda.
Kamanda Chatanda amewataka wananchi kuacha kujihusisha na biashara za magendo ikiwemo uuzaji wa dawa ya kulevya aina ya heroin pamoja na mirungi.
Amesema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha biashara hizo haramu zinakomeshwa na kuwataka watu kutoa taarifa pindi wanapowatilia shaka wengine.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania