December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Fyandomo awataka wanawake kuacha uoga

Na Esther Macha, TimesmajiraOnline,Chunya

MBUNGE wa viti Maalum Mkoa wa Mbeya,Suma Fyandomo amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele kugombea nafasi zozote zinapojitokeza na wasisite wala kuogopa kwani wao ni jeshi kubwa na nguzo katika familia.

Fyandomo amesema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani kiwilaya yaliyofanyika katika kijiji cha Ifuma Kata ya Lupa Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya.

Fyandomo amesema wanawake wana uwezo mkubwa hivyo ni vyema kujitokeza kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwani hawashindwi kutekeleza majukumu mbalimbali ya kifamilia, kijamii hivyo hata kwenye uongozi wanaweza pia.

“Naamini sisi wanawake ni wa kitaifa tuna uwezo mkubwa hebu tuamke sasa na kutiana moyo na kuondoana hofu na sasa tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa hima tujitokeze kwa wingi msingi mzuri tuanzie huku tutafika mbali kuliko tunavyofikiria “amesema Fyandomo.

Aidha amesema kuwa ni wakati sasa kwa wanawake kuchangamkia fursa mbali mbali zinapojitokeza mbele yao na kuacha woga ujasiri iwe ndiyo nguzo kubwa kwao.

“Wanawake tuna uwezo mkubwa sana tukiamua hivyo na Mimi nawahimiza tusonge mbele kwani tuna uwezo wa kukabili mambo mengi hata kwenye familia zetu hivi tujiamini na kuwa kitu kimoja “amesema Fyandomo.

Akisoma risala kwa Mgeni rasmi katibu wa kamati ya maandalizi ya siku ya Wanawake duniani wilaya ya Chunya,Bahati Mwampetele amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imefanya jitihada mbalimbali katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwawekea mazingira wezeshi ya biashara pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kupinga vitendo vya ukatili , kutoa elimu ya malezi na makuzi ili kuwajengea wanawake uwezo wa kujiamini.