Na Mwandishi wetu
SHIRIKA linalojihusisha na kuleta ushawishi wa kuchukua hatua kustahimili na kupunguza athari za Mabadiliko ya Tabia ya nchi(FORUMCC), imeipongeza Serikali kupitia Bajeti yake ya fedha 2020/2021 kwa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme utokanao na jotoardhi katika mto Ngozi-Mbeya ifikapo 2021.
Akitoa maoni ya Shirika hilo kuhusu Bajeti iliyowasilishwa Bungeni hivi karibuni katika upande wa masuala ya Nishati, Mkurugenzi wa FORUMCC, Rebecca Muna amesema, hiyo ni moja ya njia nzuri ya Serikali kuanza uwekezaji wake katika matumizi ya nishati mbadala nchini.
Amesema, bajeti ya mwaka huu imegusia vizuri masuala ya nishati jadidifu tofauti na miaka ya nyuma iliyopita kwani awali nishati ya upepo, jua na jotoardhi uchangia asilimia 3.8 tu ya kiwango cha nishati mbadala nchini.
“Tunaipongeza Serikali kwa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme utokanao na jotoardhi katika mto Ngozi-Mbeya ifikapo 2021. Uzalishaji huo utachangia Megawati 30 katika jumla ya umeme unaozalishwa nchini pia, Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kuzalisha umeme (MW 2.4) kutokana na nguvu ya upepo katika wilaya ya Mufindi-Iringa na kuanza kwa ujenzi wa mradi wa kihistoria wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2,115) katika mto Rufiji hii inaonyesha kwa namna gani Serikali hii imejipanga na kuweka nguvu katika kuimarisha nishaji jadidifu,”.
“Mwezi Septemba 2018, Serikali kupitia TANESCO ilitangaza fursa kwa wawekezaji binafsi katika miradi ya nishati jadidifu (Jua – MW 150 na Upepo – MW 200) lengo ni kupata miradi ya kuzalisha umeme wa jumla ya MW 950 kwa njia ya ushindani na kuingizwa katika Gridi ya Taifa,” amesema Rebecca.
Amesema, FORUMCC chini ya Mradi wake wa masuala ya nishati jadidifu unaofadhiliwa na Shirika la Hivos imekuwa ikisaidia kusisitiza wadau mbalimbali umuhimu wa utumiaji wa nishati mbadala na kushauri serikali kuhakikisha masuala ya nishati jadidifu yanapewa kipaumbele ili kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mratibu wa Miradi wa ForumCC, Henry Kazula amesema, shirika lao na wadau mbalimbali wamekuwa mstari wa mbele kuishauri serikali kuhusu maboresho ya Sera na Uwajibikaji katika kuboresha hali ya upatikani wa nishati rafiki kwa mazingira na jumuishi ili kuchangia juhudi za kukabiliana na athari za Mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Afisa Miradi wa Shirika hilo, Sara Pima amesema kuwa, wamekuwa wakielimisha jamii na kuwajengea uwezo asasi za Kiraia kuhusu fursa zilizopo za kiuwekezaji kupitia matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira katika kuzalisha mazao ya chakula na biashara.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa