MKOA wa Lindi kihistoria sio wa kiufugaji ma wafugaji wachache waliopo hufuga zaidi mbuzi, kondoo, kuku, bata, kanga, njiwa na ng’ombe ambao kwa uchache sana na mara nyingi hutumiwa kwa kitoweo, shughuli za biashara, kimila na utamaduni.
Mara baada ya baada ya Serikali ya Mkoa huo kukubali kupokea mifugo toka Mikoa mingine yenye idadi kubwa ya ng’ombe, sekta ya mifugo imeendelea kukua na kuongeza mwamko kwa wananchi katika kujiletea maendeleo yao.
Mkoa wa Lindi hadi kufikia Machi, 2018 una jumla ya ng’ombe wa asili 118,760, mbuzi asili 79,183, mbuzi wa kisasa 8,138, na kondoo 9,007, ngamia 10, Nguruwe 5,166, kuku 1,460,491, punda 121, kanga 5,788, bata maji 25,111, bata mzingi 112, Njiwa 1,586 na Sungura 212.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Mkoa, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi 2018 fedha zilizotokana na biashara ya mifugo katika Halmashauri zote mkoani humo zilikuwa ni zaidi ya Tsh. Bilioni 5.1 zilizotokana na ushuru wa machinjio, leseni za wafanyabiashara wa nyama pamoja na usafirishaji wa mifugo.
Pamoja na sekta hiyo kuwa chanzo muhimu cha mapato katika Mkoa huo, bado kuna msukumo mdogo wa Serikali katika uendelezaji wa miundo mbinu ya mifugo ikiwemo machinjio, maeneo kwa ajili ya malisho, maeneo ya malambo kwa ajili ya mifugo, majosho pamoja na uchache wa mashamba ya mifugo.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi inatekeleza ujenzi wa mradi wa machinjio ya kisasa katika eneo la Ngongo unaolenga katika kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ikiwemo nyama ambayo mahitaji yake yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku mkoani humo.
Halmashauri hiyo hadi sasa imetumia kiasi cha Tsh Bilioni 1.4 zilitolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya kukamilisha mradi huo, ambao ni moja ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Halmashauri hiyo ili kuiwezesha kujitegemea kimapato katika utoaji wa huduma zake kwa wananchi.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Maafisa kutoka Idara ya Habari (MAELEZO) waliofanya ziara hivi karibuni mkoani humo, Mhandisi Godfey Msoma wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, anasema mradi huo ulioanza mwaka 2017 umekamilika kwa asilimia 98, ikiwemo awamu muhimu mbili za mwanzo zinazohusisha jengo la machinjio pamoja na miundombinu yake.
Anaongeza kuwa mradi wa machinjio hayo pindi utakapokamilika utaweza kutoa huduma ya kuchinja ng’ombe 100, mbuzi 100 kwa siku na hivyo kufungua milango ya uwekezaji mkubwa na wenye tija kwa kwa wafugaji na wafanyabiashara mkoani huo pamoja na Mikoa jirani katika Ukanda wa Kusini.
‘’Kwa Manispaa ya Lindi, hii ni fursa na tutatumia mradi huu kwa ajili ya kuhamasisha wananchi wetu wafuge kisasa kwani kwa kufanya hivyo kutawawezesha kujiongezea fursa ya masoko kwa mifugo yao na kuweza kufanya minada ya mifugo yao na pia kuuza bidhaa za nyama zenye ubora wa kimataifa’’ alisema Msoma.
Aidha Msoma alisema malengo ya ujenzi wa mradi huo ambao pia ni miongoni mwa miradi mikubwa ya uwekezaji katika Halmashauri hiyo ni kukidhi mahitaji makubwa ya machinjio ya kisasa katika Ukanda wa Kusini kutokana na ukweli kuwa mikoa hiyo kwa sasa inaendelea kupokea makundi makubwa ya wafugaji wa kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Msoma anasema ili kuhakikisha machinjio hayo yanakuwa ya kisasa na endelevu, mradi huo pia utahusisha ujenzi wa nyumba ya Daktari wa wanyama ambaye atakuwa na jukumu la kufanya ukaguzi na uhakiki wa ubora wa nyama inayozalishwa kabla ya kumfikia mlaji ili kuhakikisha kuwa afya za walaji zinalindwa kwa manufaa ya jamii husika.
‘’Machinjio haya ni ya kisasa kabisa katika ukanda wa kusini, malengo yetu ni kuhakikisha tunakidhi viwango vya kimataifa katika uzalishaji wa nyama bora ili kuweza kupanua mahitaji ya soko la bidhaa za nyama kimkoa, kitaifa na kimataifa, hivyo tumepanga kuhakikisha kuwa miundombinu yake inakuwa na sifa zinazostahiki’’ anasema Msoma.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri hiyo, Dkt. Iddi Nizari ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ambao umejengwa katika viwango vya kimataifa kwa kuwa utasaidia kuongeza mapato ya Mkoa wa Lindi na taifa kwa ujumla.
Anaongeza kuwa ujenzi wa mradi wa machinjio hayo unatarajia kuongeza chachu ya uwekezaji kwa wafugaji na wafanyabiashara wa nyama mkoani humo kwani utaweza kuhudumia wanyama wengi na hivyo kutoa fursa ya kufanyika kwa minada mikubwa katika Ukanda wa Kusini.
‘’Machinjio haya yatazalisha nyama bora zinazouzwa katika maduka mbalimbali na pia kupanua soko letu la nyama katika nchi za nje kwani watumaji wengi wa nyama waliopo nje ya nchi wanaopenda kuona bidhaa iliyozalishwa katika viwango vyenye ubora na hili kwa upande tumejipanga katika kufikia viwango hivyo’’ alisema Dkt. Nizari.
Akifafanua zaidi Dkt.Nizari anasema ujenzi wa machinjio hayo utasaidia kutoa hamasa kwa wafugaji mkoani humo kufuga kisasa zaidi hatua itakayowezesha kuongeza tija ya uzalishaji wa bidhaa ya nyama mkoani humo kuweza kufikia mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
‘’Machinjio tunayoitumia sasa ni ndogo sana lakini pia haina ubora wa kuhudumia mifugo yetu kwa mfano machinjio tunayoitumia kwa sasa katika Halmashauri yetu ina uwezo wa kuchinja ng’ombe 10 na mbuzi 20 kwa siku, hivyo bado hatujaweza kufikia malengo tuliyojiwekea katika Halmashauri’’ anasema Dkt. Nizari.
Aidha Wananchi mbalimbali katika Manispaa ya Lindi walitoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa ujenzi wa mradi huo, ambao wanaueleza utakuwa mkombozi kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kusini kwani utafungua milango ya kiuchumi na kuimarisha sekta ya mifugo katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Mmoja wa Wananchi wa Kata ya Tulieni, Manispaa ya Lindi Bw. Bakari Mchukuma anasema ujenzi wa machinjio ya kisasa utasaidia kuondokana na ufugaji wa kimazoea kwani hapo awali walikuwa na mifugo mingi katika jamii yao ikiwemo ng’ombe ambao wilitumika katika shughuli mbalimbali za kimila ikiwemo ngoma za asili zinazofanyika kila mwaka mara baada ya kumalizika kwa msimu wa kilimo.
‘’Mkoa wetu haukuwa mkoa wa kifugaji, tulikuwa na ng’ombe, Mbuzi, kondoo, kuku na mifugo mingine ambayo mingi ilitumika kwa ajili ya sherehe za kimila ikiwemo ngoma, lakini kwa sasa Serikali ya Rais Dkt. John Maguful imeamua kujenga machinjio kubwa, bora ya kisasa katika manispaa ya Lindi, ambayo itatusaidia kuiuza na kupata pesa kwa ajili ya kuendesha maisha yetu’’ anasema Mchukuma.
Aidha Mchukuma aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa mradi huo kwani utasaidia kuongeza idadi ya minada ya mifugo Mkoani humo, ambapo kwa sasa kuna jumla ya minada minne tu ambapo kati ya hiyo, minada miwili inapatikana Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, mnada mmoja uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi huku Halmashauri ya Lindi pia ikiwa na mnada mmoja.
Kwa upande wake Abdul Kasembe Mkazi wa kijiji cha Mitandi Manispaa ya Lindi, ambaye ni mfugaji anayemiliki ng’ombe 30, mbuzi 45 na kondoo 25, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa mradi wa machinjio hayo kwa kuwa umedhihirisha dhamira ya Rais Dkt. John Magufuli ya kusaidia wananchi wa kipato cha chini katika kujikwamua kiuchumi.
Anaongeza kuwa kwa upande wake machinjio hayo yamempa fursa ya kufuga kisasa, kwani ataweza kuiuza mifugo yake katika minada mikubwa inayotambulika na Serikali na kuwasaidia kulanguliwa na wafanyabiashara wasio waaminifu.
Naye Emmanuel Kwaang, mkazi wa kijiji cha Matopeni Manispaa ya Lindi ambaye pia ni mfugaji wa mbuzi na kondoo anasema uwepo wa machinjio hayo utasaidia kupatikana kwa soko la uhakika wa mifugo mkoani humo, ukilinganisha na hali ilikuwapo hapo awali ambapo walikuwa wakisafiri hadi mikoa ya jirani ikiwemo Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kutafuta masoko.
Kwaang aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo kwa kuwa utasaidia upatikanaji wa masoko ya uhakika wa mifugo yao sambamba na kupunguza umbali wa kusafirisha mifugo yao, ambayo hupungua thamani pindi wanapoenda kuiuza katika minada iliyopo nje ya Mkoa huo.
‘’Nampongeza Rais Dkt. John Magufuli kupitia Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa machinjio haya kwani imetusaidia sana sisi wafugaji kuweza kupata soko la uhakika la kuuzia mifugo yetu na hivyo kuweza kuchangia pato la Mkoa wetu wa Lindi kutokana na Kodi tutakayoanza kuilipa pindi machinjio haya yatakapoanza kufanya kazi’’ anasema Kwaang.
Naye Hamis Mohamed mfanyabiashara wa bidhaa za nyama na Mkazi wa RahaLeo Manispaa ya Lindi, anasema ujenzi wa machinjio hiyo utawasaidia kuongeza wigo wa biashara yake Mkoani humo na mikoa ya jirani kutokana na ubora wa nyama itakayozalishwa kiwandani hapo kuwa ni yenye ubora na hivyo kufungua milango ya ushirikiano wa biashara baina ya Tanzania na nchi jirani ikiwemo Msumbiji.
‘’Pindi machinjio haya yakikamilika na kuanza kazi yatasaidia kupanua mtandao wa biashara baina yetu na mataifa jirani ikiwemo nchi ya Msumbiji, na kufanya hivi kutasaidia kuongeza kodi ya serikali naipongeza serikali ya Awamu ya Tano kwa kubuni mradi huu ambapo utafungua fursa ya ukuaji wa biashara kwa mikoa ya ukanda wa kusini’’ anasema Mohamed.
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inatekeleza Mkakati Maalum unaolenga kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwemo Halmashauri kujitegemea kimapato ili kutoa huduma bora zaidi na zenye uhakika kwa wananchi.
Kwa kuzingatia sababu hizo, Wizara ya Fedha na Mipango imeanzisha utaratibu kwa Halmashauri mbalimbali nchini kufanya mawasilisho ya miradi yao ya kimkakati katika eneo la kujijenga kimapato kwa madhumuni ya kujitegemea na kuboresha utoaji wa huduma.
Kwa msingi huo, ujenzi wa machinjio ya kisasa katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi utasaidia upatikanaji wa mapato ya kutosha na yenye uhakika katika Halmashauri hiyo ikiwa ni nguzo imara katika kuboresha utoaji huduma nzuri na zenye uhakika kwa wananchi.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika