Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dodoma
TUME ya Ushindani (FCC) imesema kuwa biashara ya bidhaa bandia imeendelea kuwa tishio kubwa kwa uchumi wa Taifa na dunia kwa ujumla, kutokana na kuharibu mazingira ya uwekezaji, kupunguza mapato ya Serikali na kuhatarisha afya za walaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuelekea Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Udhibiti wa Bidhaa Bandia Duniani, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Salvator Chuwa, amesema bidhaa bandia zinachangia kati ya asilimia 2.5 hadi 3.3 ya biashara ya kimataifa, hali inayotoa mianya ya upatikanaji wa mapato haramu duniani.
Chuwa ameeleza kuwa bidhaa bandia zimekuwa zikiathiri kwa kiasi kikubwa ushindani wa haki katika masoko kwa kuzipa changamoto bidhaa halali zinazozalishwa na wawekezaji halisi.
Amefafanua kuwa gharama kubwa za uendeshaji na uzalishaji wa bidhaa halali haziwezi kushindana na bei za bidhaa bandia ambazo si salama na hukosa ubora, hali inayosababisha wazalishaji halali kufunga biashara, kupungua kwa ajira na mapato ya kodi kwa Serikali.
“Biashara ya bidhaa bandia ni kosa la jinai na pia ni ukiukwaji wa mikataba ya kimataifa ikiwemo ile ya Shirika la Biashara Duniani (WTO), ambayo Tanzania ni miongoni mwa wanachama. Endapo hatutadhibiti hali hii, ushiriki wetu wenye tija katika biashara ya kimataifa utaathirika,” alionya.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuelimishwa kuhusu madhara ya bidhaa bandia, ili wawe na uwezo wa kutambua, kukwepa na kutoa taarifa juu ya bidhaa hizo. Kwa mujibu wake, udhibiti huo hauwezi kuwa wa upande mmoja pekee, bali unahitaji ushirikiano baina ya Serikali, sekta binafsi, wamiliki wa miliki bunifu na wadau wa maendeleo.
Kwa upande wa utekelezaji wa majukumu ya FCC, Chuwa amesema Tume hiyo hufanya kaguzi katika maeneo ya kuingilia bidhaa nchini kama bandari, vituo vya forodha na mipakani, sambamba na kutoa elimu kwa wadau kupitia ofisi zake zilizopo Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha na Mbeya.
“Katika kutekeleza jukumu hili muhimu, FCC inashirikiana kwa karibu na jumuiya za wafanyabiashara, wataalamu wa ushuru wa forodha (TAFFA), vyuo vikuu, taasisi za Serikali na mashirika ya kimataifa ili kuhakikisha elimu inawafikia walengwa kwa upana na ufanisi mkubwa,” amebainisha.
Ameeleza kuwa Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika jijini Dodoma yakiwa na kaulimbiu “Kujenga Kesho Salama, Kutetea Uhalisia kwa Uongozi Thabiti” na kwamba Shughuli mbalimbali zimepangwa kuanzia Juni 19 hadi 25, zikiwemo vipindi vya redio, semina na Kongamano la Kitaifa litakalowakutanisha wamiliki wa miliki bunifu, wanasheria, wafanyabiashara, wanahabari na taasisi mbalimbali za Serikali na kimataifa.
Ngasongwa amesema kuwa Kongamano hilo litafanyika tarehe 25 Juni 2025 katika Ukumbi wa Mabeo, jijini Dodoma na linatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo .
Aidh ameeleza kuwa FCC imewajengea uwezo wadau wengi kupitia warsha na semina mbalimbali ikiwemo Wakuu wa Mikoa, Kamati za Kudumu za Bunge, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Makatibu Wakuu wa wizara mbalimbali, pamoja na wanachama wa vyama vya wafanyabiashara kama JWT, CTI, SHIUMA na CHAWASAPI.
Chuwa amebainisha kuwa elimu hiyo pia imewafikia wanafunzi wa vyuo vikuu zaidi ya kumi nchini pamoja na taasisi za Zanzibar (ZFCC) na Kenya (ACA), kwa lengo la kuimarisha uelewa na ushirikiano wa kikanda katika kupambana na bidhaa bandia.
Katika kuhakikisha udhibiti wa bidhaa bandia unafanyika kwa ufanisi zaidi, FCC imepanua huduma zake kwa kufungua ofisi mpya tatu za kikanda – Mwanza, Arusha na Mbeya ambazo zinafanya kazi ya kudhibiti uingizaji wa bidhaa bandia kupitia mipaka mikuu ya kibiashara kama Namanga, Kasumulu na Tunduma.




More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi