January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

FCC yazindua wiki ya ushindani kitaifa

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Tume ya Ushindani nchini (FCC) imezindua wiki ya ushindani kitaifa ambapo Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Jaffo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika siku ya Kilele cha maadhimisho hayo Disemba 5, 2024 yatakayofanyika Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) William Erio, amesema kupitia Wiki hiyo wamejipanga kutumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wadau kutoka sekta mbalimbali nchini wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu na wanasheria ili kuimarisha ushindani wa haki sokoni na kuchangia maendeleo ya Taifa.

“Tunazindua leo shughuli yetu na kuanzia siku ya jumatatu tarehe 02 na 03 December tutafanya semina kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na wanasheria ili kuwaeleza kwa kina kuhusu siku yetu hii tukijikita katika kauli mbiu yetu na siku ya tarehe 04 December tutatoa elimu kwa umma kupitia runinga na redio ambapo kilele cha maadhimisho yetu haya yatakua December 05 mwaka huu”

Erio amesema kuwa FCC wana wajibu wa kuwakumbusha wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa kuzingatia kanuni na taratibu pamoja na misingi ya ushindani na kuwaelimisha wananchi kuhusu serikali yao nini inafanya katika kuhakikisha inawalinda.

Amesema kupitia maadhimisho hayo wao kama taasisi wataonyesha namna walivyojipanga katika kuhakikisha wanaboresha mifumo na utendaji wao jambo ambalo litasaidia utekelezaji wa majukumu yao yawe mazuri zaidi na kuyawezesha makampuni na wafanyabiashara wa Tanzania kunufaika na fursa zilizopo katika soko huru la biashara la afrika na lile lililopo katika jumuiya ya afrika mashariki.

Ameongeza kuwa siku ya ushindani duniani imelenga kuelimisha jamii, wadau kutoka sekta mbalimbali kuhusu kuzingatia umuhimu wa kanuni,sera na sheria za ushindani za biashara za hapa nchini na duniani kote.

“Kanuni za biashara zinawafanya watendaji wa biashara kuwa na fursa sawa kwa wote, na sheria zetu zipo katika mambo kadhaa ambayo yanazuia vitu ambavyo vitarudisha maendeleo ya kufanya biashara” amesema Bw. Erio.

Amesema kuwa vitu ambavyo sheria inakataza ni pamoja na kupanga bei za bidhaa wanazofanya, kupunguza uzalishaji, kugawana zabuni pamoja na kula njama ambayo itapelekea kurudisha nyuma maendeleo ya ushindani.

FCC ina jukumu la kuboresha mifumo na utendaji wake ili kuimarisha ushindani katika soko, jambo ambalo litawanufaisha wafanyabiashara na makampuni ya Tanzania kwa kutumia fursa zilizopo katika soko huru la biashara barani Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, kauli mbiu ya mwaka huu ambayo inasema ‘ Sera ya ushindani inavyoweza kutumika katika kupunguza utofauti wa usawa katika ufanyaji biashara’ inahimiza matumizi ya sera ya ushindani kama nyenzo ya kupunguza utofauti wa usawa katika biashara.

Wiki hii ya Ushindani ni fursa muhimu kwa wadau wote kujifunza na kuelewa nafasi yao katika kuchangia maendeleo ya ushindani wa haki nchini, kwa manufaa ya uchumi na ustawi wa Taifa