Na Jackline Martin, TimesMajira Online
TUME ya Ushindani (FCC), imesaini mkataba wa ushirikiano na Taasisi ya Trademark Afrika (TMA) wenye thamani ya sh. bilioni 1.5, kwa awamu ya kwanza wenye lengo la kukuza uchumi wa biashara nchini na kuhakikisha shughuli zote za kiutendaji zinafanyika kupitia mifumo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa FCC, William Erio alisema, mkataba huo wa miaka mitatu ulianza kufanya kazi Novemba mwaka jana.
Erio alisema mkataba huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili ambapo mwaka moja wataangalia matokeo yaliyopatikana ndani ya miaka hiyo miwili na kujiridhisha utendaji kazi kama ilivyokusudiwa.
Pia Erio alisema fedha ambazo wamepatiwa na TMA, watazitumia katika mambo matatu ambayo ni kufanya maboresho ya miundombinu ya Tehama, mafunzo kwa wafanyakazi wao na kuwekeza zaidi katika mitandao ya kidigitali.
“Tutahakikisha fedha hizi tunafanya maboresho makubwa kwa lengo la walaji ili wasipate tatizo, pia kuhakikisha Tanzania inakuwa kiuchumi,” alisema Erio.
“Unaweza ukawa na miundombinu mizuri, ukawa na kilakitu kilichokamilika lakini kama watumiaji wa mifumo hawaielewi vyema, ufanisi tunaoutarajia hautakuwepo hivyo tutahakikisha wafanyakazi wa FCC wanapata elimu ya kutosha” Aliongeza
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TMA, Elibariki Shammy alisema mkataba huo utakuwa endelevu, kufuatilia eneo la sera ya biashara kuwezesha Tanzania kupata fursa ya uwekezaji.
Alisema lengo la kushirikiana na FCC ni kuhakikisha eneo la sera linakuwa bora na kutanua wigo mpana wa biashara ngazi ya kimataifa.
“Dunia inakuwa kwa kasi ndiyo maana tumeshirikiana na FCC katika kuhakikisha Tanzania inapiga hatua katika soko la biashara, kuwakaribisha wawekezaji,”
Shammy aliongezea kuwa mkataba unaokuja utakuwa na nguvu zaidi kwa lengo la kufungua fursa ya biashara kimataifa.
“Takwimu za Dunia zinaonyesha kuwa mwaka 2017 zaidi ya Dola Bilioni 500 Duniani zimepotea kwa makampuni Yale yanayofanya kazi kwa uhalali, hivyo ushirikiano huu utasaidia kukuza biashara na kusisimua uwekezaji”
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja