May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

FCC na ZFCC wakutana na kupanga mikakati kuzuia bidhaa bandia

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

TUME ya Ushindani Tanzania (FCC) kwa kushirikiana na Tume ya Ushindani Halali ya Zanzibar (ZFCC) zimejipanga kudhibiti uingizaji na uzalishaji wa bidhaa bandia ili kuchochea uchumi utakaolinda soko la ndani pamoja na mlaji.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mkuu FCC, William Erio wakati wa kuhitimisha ziara ya kikazi ya siku tatu ya maofisa wa ZFCC waliotembelea FCC kwa lengo la kuimarisha mahusiano na kuangalia namna bora ya kutekeleza majukumu yao.

“Suala la biashara si suala la muungano, kwa hiyo sisi FCC tunashughulika na masuala haya ya kibiashara kwa maana ya kushajihisha ushindani, kulinda washindani katika shughuli zao na kumlinda mlaji kwa
Tanzania bara, ambapo na wenzetu wanafanya hivyo hivyo kwa upande wa Tanzania Zanzibar,”alisema na kuongeza;
“Pamoja na kwamba suala la biashara si suala la muungano, lakini muingiliano kibiashara kati ya pande hizi mbili ni mkubwa, kwanza kwa wafanyabiashara wenyewe lakini pia wawekezaji ambao wamewekeza
katika pande zote mbili za muungano”

Aidha Mkurugenzi huyo alisema Serikali ya awamu ya sita imejikita katika kuimarisha uwekezaji kama njia mojawapo ya kuleta mitaji na kukuza uchumi wa nchi yetu.

Pia Erio alisema wanajipanga zaidi kuhakikisha nchi inanufaika na soko la Afrika Mashariki kwa sababu sisi wote ni sehemu ya Afrika mashariki.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu ZFCC, Mohammed Sijamini Mohammed alisema Zanzibar inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kufanya mapitio ya baadhi ya sheria ikiwemo sheria ya
maendeleo ya viwanda ambayo itawezesha wananchi kunufaika na bidhaa zinazozalishwa viwandani.

“Kwa upande wa Zanzibar kuna jitihada kubwa zinafanyika za makusudi kwake Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuweka mazingira bora ya biashara na kudhibiti ushindani”

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani wa Kibiashara  (FCC) Bw. William Erio akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha kikao kati ya taasisi hiyo na Tume ya Ushindani Halali ya Biashara ya Zanzibar (ZFCC) kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Halali wa Biashara Zanzibar (ZFCC) Mohammed Sijamini Mohammed.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Halali wa Biashara Zanzibar (ZFCC) Mohammed Sijamini Mohammed akizungumza katika kikao hicho kati ya taasisi hiyo na Tume ya Ushindani wa Kibiashara  (FCC) , kushoto ni Mkurugenzi Miungano ya Makampuni na Udhibiti wa Ushindani (ZFCC) Ummy Muhamed Rajab