November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Familia zatakiwa kuwafundisha watoto wa kike kuhusu hedhi salama

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Dar-es-salaam

FAMILIA zimetakiwa kutoa elimu ya hedhi salama kwa watoto wa kike na zione ni sehemu ya maisha ya watoto hao ili waweze kuona hali hiyo ni jambo la kawaida.

Rai hiyo imetolewa leo Julai 6,2024 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe wakati wa kongamano la Kitaifa la wadau wa sekta ya Afya kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere(JNICC).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe

‘’ Familia zisaidie watoto wa kike kwa ujumla katika utoaji wa elimu ya hedhi salama ili kujiandaa kisaikolojia na waone ni kitu cha kawaida katika makuzi yao,’’ amesema.

Dkt.Magembe amesema Kampeni ya Mtu Ni Afya, inaendana sambamba na uandaaji wa dira ya maendeleo 2050.

‘’Ili tuweze kuwa na maendeleo yoyote, lazima tuwe na afya bora huwezi kuwa mtu umekamilika kama wewe ni mgonjwa,’’ amesema.

Pia amesema kampeni hiyo inaongelea usafi wa mazingira ikiwemo matumizi ya vyoo safi pamoja na maji safi na salama.

Katika hatua nyingine, ameitaka jamii kuepeuka matumizi ya vilevi kama pombe pamoja na kutumia chumvi nyingi iliyopitiliza.

Ameshauri pia jamii iwe na mtindo bora wa maisha pia ni lazima kufanya mazoezi ya mwili ili uwe salama.

Naye Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema mipango ya serikali ni kuwa kila Mtanzania ifikapo 2050 ni lazima awe na afya bora.

‘’ Kwenye sekta ya afya, tunaguswa sana na masuala lishe, jukumu letu ni kuhakikisha upatikanaji wa afya bora kwa watu wote na kuzingatia upatikanaji wa maji safi na salama,”’ amesema.

Pia ameitaka jamii kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi na kuzingatia ulaji mzuri wa chakula.

Amesema licha ya juhudi mbalimbali zilizofanywa na serikali katika kuboresha sekta ya afya bado kuna tatizo kubwa la magonjwa yasioambukiza ikiwemo shinikizo la damu,kisukari na afya ya akili.

‘’ Tumefanya vizuri kama Sekta ya Afya katika miaka 25 iliyopita ila bado ipo kazi kubwa tunatakiwa tufanye ili tuweze kufikia lengo la afya bora kwa wote,’’ amesema.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akitoa maada wakati wa kongamano la kitaifa la wadau wa sekta ya Afya kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

Kwa upande wake Ofisa Muuguzi wa Zahanati ya Makumbusho jijini Dar-es-Salaam, Judith Mwakipesile amesema jamii inatakiwa kujali afya kuanzia nyumbani mpaka mazingira ya kazini.

‘’Ukiingia katika zahanati yetu unakutana na sehemu ya kunawia mikono pia kuna ndoo za kutupa takataka zilizotenganishwa na kuna vitakasa mikono sehemu mbalimbali,”amesema.

Amesema katika vyoo vya zahanati yao kuna maji tiririka huku kuhusu suala la hedhi, Mwakipesile amesema ni jukumu la wazazi wote wawili kuwafundisha watoto wa kike.

Baadhi ya washiriki wakiwa katika kongamano la kitaifa la wadau wa sekta ya Afya kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050