January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Failuna, Geay mzuka wote mbio za kimataifa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

NYOTA wa kimataifa wa Tanzania katika mchezo wa riadha, Failuna Matanga na Gabriel Geay
wapo katika maandalia makali ili kuhakikisha wanaiwakilisha vema nchi katika mashindano ya kimataifa ya riadha yatakayofanyika mwishoni mwa mwezi Novemba na Mwanzoni mwa Desemba.

Katika mashindano hayo, Failuna atatupa katara yake Novemba 29 nchini India katika mbio za New Dehil wakati Geay anatarajia kushiriki mbio za Valencia zitakazofanyika Desemba 6.

Hayo yatakuwa mashindano ya kwanza ya kimataifa nyota hao kushiriki toka walipokwama kwenda nchini Poland kwa ajili ya kuiwakisha nchi katika mashindano ya Dunia ya riadha ya ‘World Half Marathon’ yaliyofanyika Oktoba 17.

Safari hiyo iliyeyuka huku ikiwa tayari walishafanya usajili na kwanza na walikuwa wanasubiri kukalimika kwa mchakato wa tiketi ili waweze kuthibitisha ushiriki wao katika mashindano hayo.

Kocha anayesimamia mazoezi ya nyota hao, Thomas Tlanka ameuambia Mtandao huu kuwa, mazoezi wanayoendelea nayo nyota hao ni mwendelezo wa yale waliyoanza kuyafanya kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo ya kimataifa.

Amesema, licha ya mashindano hayo kuota mbawa kwao, lakini hawakuwa na sababu ya kusitisha mazoezi kwani tayari walishakuwa na mapango wa kushiriki mashindano mengi zaidi ya kimataifa ikiwemo hiyo ya Valencia na New Dehil.

Kwa sasa anachoendelea nacho ni kuwapa mazoezi zaidi yatakayowaongezea morali ya kupambana zaidi kwani tayari walishaona ubora wao katika mashindano ya Ngorongoro yaliyofanyika mwezi uliopita.

Katika mashindano hayo ambayo yaliyatumia kama sehemu ya kuimarisha viwango vya wanariadha hao, Geay aliibuka kinara kwa upande wa wanaume akitumia saa 1: 4 : 42 na kuvunja rekodi iliyowekwa mwaka jana na Abraham Too kutoka Kenya, aliyetumia saa 1: 5: 59 na kumshinda Herman Sule kutoka Mbulu aliyetumia 1: 6: 10 na Josephat Joshua kutoka Polisi Tanzania aliyetumia saa 1: 6: 57.

Kwa upande wa wanawake, mshindi wa jumla alikuwa Failuna kutoka klabu ya Talent ya Arusha aliyetumia saa 1: 16: 3 akimpuki mshindi wa mwaka jana Esther Chesang kutoka Kenya aliyetumia saa 1:16:49 huku nafasi ya pili Natalia Sule kutoka klabu hiyo akitumia saa 1:16:43.

Kocha huyo amesema, kutokana na hamu kubwa ya mafanikio wanayoitaka wanaridha hao kimataifa inayochagizwa na mikakati yao ya kufika mbali, ni dhahiri wataweza kupeperusha vema bendera ya nchi kama walivyofanya kwenye mashindano yaliyopita.

“Wanariadha wetu wanaendelea vizuri na maandalizi ingawa kuna mambo machache ambayo tunapaswa kuyarekebisha, tayari tumeongeza zaidi ‘dozi’ ya mazoezi ambayo itakuwa ikiongezeka kadri siku zinavyokwenda na tunaimani jambo hilo litazidi kuwapa morali ya kufanya vizuri katika mashindano hayo,” amesema kocha Thomas.