Judith Ferdinand
Kipindupindu ni ugonjwa hatari sana wa mlipuko unaosababishwa na vijidudu aina ya bakteria aina ya Vibriocholerae.
Namna unavyoambukizwa
Akitoa elimu kwa waandishi wa habari, Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Mwanza, Renard Mlyakado, ameeleza kuwa ugonjwa wa kipindupindu una ambukizwa kwa kunywa maji au kula chakula kilichochafuliwa na kinyesi chenye bakteria wa maambukizi ya ugonjwa huo.
Nini dalili za ugonjwa wa kipindupindu
Mlyakado ameeleza kuwa dalili za ugonjwa huo huanza kuonekana ndani ya masaa 24 hadi siku tano baada ya kuambukizwa.
Ambapo dalili hizo ni kuharisha maji maji yanayofanana na maji ya mchele, kutapika, kujisikia mlegevu na kukosa nguvu, kusikia maumivu ya misuli,upungufu wa maji mwilini pia ngozi kusinyaa, midomo kukauka, macho kudumbukia ndani.
Namna ya kujikinga na kipindupindu
Anaeleza kuwa ugonjwa wa Kipindupindu unazuilika iwapo kila mwana jamii atafuata kanuni za afya hususani usafi binafsi na usafi wa mazingira.
Pia kutumia maji safi na salama (jamii kutumia maji ya kunywa yaliyochemshwa au kutibiwa (Acqua tabs), kuchujwa kwa kitambaa safi na kutunzwa katika hali ya usafi.
Vile vile kuzingatia atumizi sahihi ya choo,kunawa mikono mara kwa mara hasa baada ya matumizi ya choo,kutumia vyakula vya moto.
Pamoja na kuosha kwa maji safi vyakula vinavyoliwa bila kupikwa kama matunda, mbogamboga,kuosha vyombo vya chakula kwa maji ya moto na kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji.
” Vijidudu vya ugonjwa wa kipindupindu vinatoka kwenye kinyesi kibichi na vinasambazwa na mtu mwenye ugonjwa huo, hivyo ili kuepuka tunashauri kila mtu kuzingatia usafi suala ambalo linaenda sambamba na kula chakula kikiwa cha moto,”anasema Mlyakado
Je ugonjwa wa kipindupindu unatibika
Mlyakado anaeleza kuwa ugonjwa wa Kipindupindu unatibika endapo mgonjwa atawahi katika kituo cha kutolea huduma pia ni
rahisi kuambukizwa, ni rahisi kujikinga na ni rahisi kupoteza maisha.
Je maji yaliokaa muda mrefu na ya kwenye friji ni salama
Akizungumza dhana iliyojengeka ndani ya jamii kuhusu maji yaliokaa muda mrefu kwenye vyombo vya kuhifadhia maji ambayo hayaja chemshwa kuwa ni salama na hayawezi kusababisha kipindupindu Mlyakado anaeleza kuwa dhana hiyo siyo sahihi.
Kwani maji ambayo hayaja chemshwa na kuhifadhiwa muda mrefu,yasiyochemshwa vizuri na yaliowekwa kwenye friji bila kuchemshwa au kuwekewa dawa ya kuwa vijidudu sio njia sahihi ya kuua hao wadudu bali ni njia yao wao kuwatunza na kuwasaidia kuzaliana na mtu anapoyatumia atapata maambukizi yaleyale.
” Njia sahihi ya watu kujikinga na kuepukana na ugonjwa wa kipindupindu ni kuhakikisha wanachemsha maji na yachemke kama inavyotakiwa ili kuua wadudu wote wanaosababisha ugonjwa huo,”aneleza.
Yusuph Yusuph Mtaalamu kutoka Wizara ya Afya anaeleza kuwa vijidudu hivyo hukaa kwenye mfumo wa maji taka na pale mfumo huo unapoharibika na kuchangamana na mfumo wa maji safi ya kunywa na mtu akayatumia maji hayo bila kuyachemsha ndipo huanza kuugua ugonjwa huo.
“Bakteria wapo katika mazingira tunayoishi wakiingia kwa binadamu wanaleta madhara maana siyo sehemu yake ya kuishi,tofauti tunakuna nao wapi na lini moja ni mfumo wa maji safi kuingiliana na maji taka kwaio mtu wa kwanza anaweza kuanzia hapo na wa pili hivyo ndivyo mzunguko wa kuambukizana unavyokuwa,”anaeleza Yusuph.
Hivyo anaishauri jamii kuhakikisha maji ya kunywa yanachemka au kutibiwa,watu wale vyakula vya moto,usafi uzingatiwe wakati wa maandalizi ya chakula kwa kuhakikisha kinaandaliwa katika mazingira safi,kunawa mikono wakati wa kuandaa chakula na kuosha matunda vizuri na maji ya moto na chakula kikiiva kiliwe kikiwa cha moto.
Emmanuel Mnkeni ni mtaalamu wa afya kutoka Wizara ya Afya Dodoma, anaeleza kuwa bakteria hao wanashambulia mfumo wa chakula wa binadamu ambapo mtu anaanza kupata dalili ikiwemo kuharisha ambapo mtu akijisaidia maeneo ambayo ni ya mtaani au vichakani siyo kwenye choo na kama ana maambukizi ya kipindupindu mwisho wa siku mvua ikanyesha inaondoa kile kinyesi na kupeleka katika vyanzo vya maji.
Hivyo mwisho wa siku mtu akinywa maji bila kuyatibu anaweza kupata kipindupindu ndio maana wanasisitiza watu watumie maji yalio safi na salama kwa kuchemsha.
“Yote yanatokea kwa sababu mazingira yetu tunayachafua ndio maana tunasisitiza suala la mazingira kuzingatiwa ikiwemo matumizi ya choo sahihi na kwa vyoo vya shimo viwekewe mfuniko ili nzi wasiingie ndani ya choo na kubeba vimelea wa bakteria wa kipindupindu na kusambaza kwa watu,bakteria hao wapo sehemu mbalimbali ila sisi tunapata kupitia njia ya kula chakula ambacho kimechafuliwa na bakteria hao kama matunda,chakula au maji ambayo hujayatibu ili kuua vimelea vya ugonjwa huo,”anaeleza Mnkeni.
Amesisitiza kuwa ugonjwa huo unatokana na mazingira ambayo siyo safi kupitia kinyesi kibichi ambacho kimechafua aidha maji ya kunywa,matunda au chakula.
Hivyo amewataka wananchi kuhakikisha wanasafisha mazingira yao vizuri huku akiziomba Mamlaka za maji kuangalia mifumo yao ya maji ili kusaidia kudhibiti tatizo hilo.
Aidha amesisitiza kuwa mgonjwa mwenyewe ugonjwa huo asipopata matibabu kwa muda hupoteza maji mengi kutokana na kuharisha au kutapika hali ambayo inaweza kusababisha kifo.
Nini mkakati wa Mkoa katika kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu
Akizungumza wakati akifunga semina ya siku moja juu ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa waandishi wa habari jijini Mwanza iliofanyika Januari 16,2024, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachunzibwa amewataka waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na ofisi yake kwa kuelimisha jamii ili kujikinga na ugonjwa huo.
Ambapo ameeleza kuwa takribani watu 80 wameripotiwa kuumwa ugonjwa wa kipindupindu tangu Mkoa wa Mwanza ulivyoripotiwa kuwa na mlipuko wa ugonjwa huo Januari 4,2024.
Huku akieleza kuwa mkakati uliopo ni jamii kuwa na vyoo na kuzingatia matumizi yake kwa usahihi ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu kwa kila kaya kuwa na choo na kukitumia kwa usahihi.
Mkakati mwingine ni kuwahimiza wananchi kunawa mikono kwa maji safi na salama yanayotiririka na sabuni kabla na baada ya kula au kutoka chooni na kuhakikisha anakula chakula cha moto.
“Tuhakikishe kila kaya inatumia maji ambayo yapo katika chombo safi na salama,yachemshwe na kuchujwa na kitambaa safi na yawekwe kwenye ndoo ambayo ina koki hatushauri sana kikombe cha kuchotea kinaweza kuleta madhara kwani maji yanaweza kuchafuka tena,”anaeleza Dkt Rutachunzibwa.
Pia ameeleza kuwa mkakati mwingine katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo ni kuhamasisha jamii kunywa maji yaliotibiwa kwa kutumia kidonge kinachosambazwa kwa sasa kinachojulikana kwa jina la Aqua tabs.
“Kidonge hiki kinatumika kutibu maji ya ndoo ya lita 10 kidonge kimoja na kwa ndoo ya lita 20 vidonge viwili kisha unatikisa ili kuchanganya maji vizuri kidonge hichi kinatakiwa kuhifadhiwa sehemu isiyokuwa na mwanga mkali kwakuwa kikiachwa hapo kinaweza kusababisha madhara mengine ya kiafya,” amesema Dk Ruchunzibwa.
Aidha wanasisitiza watu kula chakula cha moto ikiwemo wanaopenda kula mahindi ya kuchoma barabarani ni vyema yakawa ya moto na si ya baridi kuchukua hatua kama zile zilizofanyika kipindi cha UVIKO-19.
Sanjari na hayo wanashauri kwenye jamii unapotokea msiba ni vyema kuita wataalamu wa afya ili kujiridhisha kifo kimetokana na nini,ili ikithibitika ni kipindupindu maziko yatafanyika chini ya usimamizi wa wataalamu ili kuepusha jamii kusafisha na kugusa mwili ambayo inaweza kuwa hatari kupata maambukizi.
“Kukitokea msiba ambao sababu zake zina mashaka waite wataalamu waweze kufanya tathimini hicho kifo kimetokana na nini kipindupindu au la,lakini misiba yote ndani ya Mkoa wa Mwanza,tukimaliza kuzika watu watawanyike kwani hali yamikusanyiko kwenye misiba ni moja ya kichocheo cha maambukizi kusambaa, kwenye mikusanyiko mingine kama nyumba za ibada kuwe na maji safi yanayotiririka na sabuni kuwe na vyoo safi wakati wote na watu wanatumia vyoo hivyo wavitumie vizuri katika hali ya usafi,”ameeleza Dkt.Rutachunzibwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana Thomas Salala ametaka katika maeneo ya shule,taasisi na masoko kuwe na wataalamu maalumu ambao wataenda katika maeneo hayo ili kutoa elimu na kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa kuhakikisha kunakuwa na vitu vya kuweka taka na maji yanapatikana ili kuikinga jamii na mlipuko wa ugonjwa huo.
Pia kusimamia matumizi ya vyoo,uuzaji wa vyakula holela uthibitiwe pamoja na uuzaji wa vyakula maeneo yasiyo rasmi pamoja na kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha ili iweze kuzingatia usafi na kanuni za afya.
“Eneo la Buhongwa linapaswa kuangaliwa kwa umakini na kuhakikisha pamoja na kufanya biashara ila pawe na utaratibu wa usafi kwani tusipo dhibithi ukanda huo ambao una muingiliano mkubwa wa watu pamoja na shule ambazo zimezunguka tutapata madhara makubwa kuwe na vitu vya kuweka taka na maji pia usiku,”.
Naye Ofisa Usafi na Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Desderius Polle, amesema mkakati walionao kwa upande wa mazingira ni kuhakikisha mazingira yote yanaimarishwa ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa kushirikiana na vikundi au kampuni za usafi katika Halmashauri ya Jiji hilo.
“Halmashauri ya Jiji la Mwanza ina kitengo cha Askari lakini kwa kushirikiana na Askari wa Jeshi la Akiba kwa ajili ya kuhakikisha wanadhibiti uchafuzi wa mazingira na wote wanaofanya biashara katika maeneo ambayo siyo rasmi,hivyo natoa rai kwa waliorudi kufanya biashara kwenye maeneo ambayo siyo rasmi warudi katika maeneo yao rasmi,”ameeleza.
Pia ametoa rai kwa wananchi kuacha tabia mbaya ya kununua vyakula katika maeneo ambayo siyo rasmi na kila mmoja atimize wajibu wake.
Mwenyekiti wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWS) Nyamagana Yohana Wanga ameshauri nguvu zielekezwe shuleni kwa wanafunzi ambao wapo mama ntilie wanawauzia chakula pia taarifa hiyo iwafikie wananchi kwa haraka kwa sababu ni dharura ili wachukue hatua za kujikinga na ugonjwa huo.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika