December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Picha ya video ya askofu Gwajima iliyofutwa na Facebook kwenye Instagram na IGTV hivi karibuni.

Facebook yasitisha, Askofu Gwajima ang’ara

CARLFORNIA, Facebook imesema haitaondoa tena kwenye mtandao wake ujumbe wenye madai kuwa virusi vya Corona (Covid-19) vilitengenezwa katika maabara na binadamu.

Kampuni hiyo imesema kuwa, hatua hiyo ni kufuatia uchunguzi unaoendelea kuhusiana na kiini cha ugonjwa wa Corona na kwamba imechukuliwa baada ya kushauriana na wataalam wa afya.

Facebook kwa muda sasa imekuwa ikijitahidi kuondoa ujumbe wenye kupotosha kuhusiana na COVID-19 tangu ulipozuka mwaka 2020.

Mwezi Desemba, mwaka uliopita Facebook ilisema kuwa, ingeondoa kila ujumbe uliyokuwa ukipotosha kuhusiana na chanjo za Corona.

Hivi karibuni Rais wa Marekani Joe Biden aliamuru uchunguzi ufanywe ili kubaini chanzo cha virusi vya corona ikiwemo uwezekano kuwa virusi hivyo vilitengenezewa kwenye maabara ya China.

Sasa Facebook imesema kuwa haitaondoa ujumbe wowote unaodai kuwa virusi hivyo huenda vilitengenezwa wakati ikiendelea kushauriana na wataalam wa afya huku shinikizo likiendelea kote duniani la kubaini iwapo virusi vya corona ni vya kutengenezwa na binadamu.

Ushindi kwa Askofu Gwajima

Hayo yanajiri ikiwa hivi karibuni Kampuni hiyo ya Facebook inayomiliki mtandao wa Instagram kufuta ujumbe wa video uliokuwa umepakiwa na mhubiri na Mbunge Mtanzania, Askofu Josephat Gwajima kuhusu virusi vya corona.

Kwenye ujumbe huo kwenye Instagram na IGTV, Askofu Gwajima alikuwa amedai kwamba janga la virusi vya corona lina uhusiano na juhudi za kusambaza teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya 5G.

Askofu Gwajima alitumia nafasi hiyo kuishauri Tanzania isiikumbatie teknolojia hiyo. Facebook ilisema ujumbe huo wa Gwajima umefutwa kwa kuwa unakiuka kanuni na masharti ya mtandaoni ya kampuni ya hiyo.

“Huwa tunazifuta taarifa za uzushi ambazo zimewaza kusababisha madhara moja kwa moja, ikiwa ni pamoja na ujumbe unaodai kwamba 5G inasababisha janga la virusi vya corona, na tunachunguza taarifa za aina hii,” msemaji wa Facebook aliiambia BBC.

“Duniani, tumefuta mamia ya maelfu ya ujumbe wenye taarifa za uzushi kuhusu Covid-19 na tumekuwa tunawaelekeza zaidi ya watu 2 bilioni kwa habari na maelezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na mamlaka nyingine za afya kupitia kituo chetu cha habari za Covid-19.”

Kwenye video yake hiyo kwenye Instagram na IGTV aliyoipakia mapema mwezi Mei, Gwajima ambaye ana mamia ya wafuasi katika mitandao ya kijamii, alikuwa amedai kwamba mlipuko wa virusi vya corona ambao chanzo chake ni Wuhan nchini China, ulianzisha oparesheni ya mtandao wa 5G na kusema kwamba cha kulaumiwa ni miale hatari kutoka kwa milingoti.

Alidai kwamba nchi zote ambazo ziliathirika vibaya ni zile zinazotumia teknolojia ya mawasialiano ya 5G.
“Wote walioathirika vibaya wana teknolojia ya 5G, hapa (Tanzania) hatuna. Ushauri wangu ni kuwa Tanzania isianzishe mawasiliano ya 5G kwa sasa hivi,” anasema.

Wazo la kwamba teknolojia ya mtandao wa 5G huenda ikawa na athari za kiafya sio geni.Lakini uvumi unaoendelezwa kuhusu uhusiano kati ya teknolojia ya 5G na virusi vya corona ni jambo ambalo limekuwa likiendelea hasa wakati nchi nyingi zinaendeleza kanuni ya kusalia ndani.

Ingawa anaamini kwamba juhudi za kueneza teknolojia ya 5G zinahusiana na mlipuko wa sasa, Gwajima bado anaamini kwamba ni kweli ugonjwa wa corona upo.

Aliwashauri wafuasi wake kufuata kanuni za afya zilizowekwa kama njia ya kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo, kunawa mikono kwa maji na sabuni, kutumia vitakasa mikono na pia kutogusana au kusalimiana kwa mkono.

“Ikiwa tutakataa kukubali hii corona inayosambazwa kwa teknolojia ya mtandao wa 5G, basi kuna watu watakaotuletea corona yenyewe,” amesema.

Dhana potofu 

Madai ya uhusiano kati ya vurusi vya corona na teknolojia ya 5G yamesemekana kutokuwa na ukweli wowote lakini hilo bado halijasitisha usambaaji ya dhana hiyo.

Shirika la Afya Duniani-WHO, lilisema kwamba virusi vya corona haviwezi kusambaa kupitia mawimbi ya redio au mitandao ya simu.

Madai haya yote ni “upuuzi mtupu ,” anasema Dkt Simon Clarke, profesa wa masuala ya seli za microbiolojia katika Chuo Kikuu cha Reading.

“Wazo kwamba 5G hupunguza mfumo wa kinga ya mwili si suala hata la kuchunguzwa,” anasema Dkt Clarke.
“Mfumo wako wa kinga ya mwili unaweza kupunguzwa na vitu mbalimbali ikiwemo mwili kuchoka siku nzima, au kwa kutokula lishe bora. Mabadiliko hayo si makubwa lakini yanaweza kukufanya uwe katika hali ya kupatwa na virusi.”
Huku mawimbi thabiti ya radio yakiwa na uwezo wa kusababisha joto, 5G si imara vya kutosha kuweza kuwatia joto watu kiasi cha kuleta madhara.

“Mawimbi ya Radio yanaweza kuvuruga saikolojia unapopatwa na joto, ikimaanisha kuwa mfumo wako wa kinga ya mwili hauwezi kufanya kazi ipasavyo. Lakini viwango vya nishati kutoka kwa mawimbi ya radio ya 5G ni vidogo sana na haviko imara kiasi cha kusababisha athari kwenye mfumo wa kinga ya mwili. Hakuna uchunguzi uliokwishafanyika juu ya hili .”

Mawimbi ya radio yanayotumiwa katika 5G na teknolojia nyingine za simu za mkononi hutumia masafa ya chini ya kiwango cha sumaku ya umeme.

Nishati yake ni ya chini kuliko hata kiwango cha nishati ya mwanga wa taa , haina nguvu kiasi cha kuharibu seli za mwili-kinyume na mionzi yenye masafa ya juu ambayo inajumuisha miale ya jua na mionzi ya kimatibabu (medical x-rays). Haiwezekani kwa 5G kueneza virusi vya corona, Adam Finn, profesa wa matibabu ya watoto katika Chuo kikuu cha Bristol anaongeza.

“Janga la sasa la virusi vya Corona lilisababishwa na virusi vinavyoambukizwa kutoka kwa mtu mmoja aliyeathiriwa kwa mtu mwingine.Tunafahamu hili ni kweli. Hata tuna virusi vinavyokuzwa katika maabara zetu, vilivyochukuliwa kutoka kwa mtu aliyekua anaugua.Virusi na mawimbi ya nishati ya umeme inayotengeneza mawasiliano ya mitandao ya intaneti na simu za mkononi hufanya kazi tofauti. Tofauti yake ni sawa na ya chaki na jibini,” anasema.