March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Exim,GF Automobile kurahisisha umiliki magari

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

BENKI ya Exim Tanzania na GF Trucks & Automobile Limited,wamesaini mkataba wa makubaliano (MoU), ili kuwarahisishia wananchi uwezo wa kumiliki magari nchini Tanzania kwa kuwapatia wateja suluhisho la kifedha.

Akizungumza katika hafla hiyo,Ofisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim Tanzania, Shani Kinswaga amesema,wateja ndio kiini cha kila kitu wanachofanya.

“Tumejizatiti kwenda mbali zaidi ya huduma za kifedha, ili kurahisisha maisha kwa wateja wetu kupitia ushirikiano huu na GF Automobile, umiliki wa gari unakuwa rahisi zaidi. Kuanzia upatikanaji wa mkopo, usajili hadi bima, kila kitu kinasimamiwa kwa urahisi ili mteja wetu aingie akiwa na hitaji na kutoka akiwa na suluhisho,”.

Kupitia ushirikiano huu, wateja binafsi na wafanyabiashara wa Exim Bank wanaweza kumiliki magari mapya kabisa kwa kuchangia kiasi kidogo cha awali, huku na marejesho mepesi ya kila mwezi kwa muda wa hadi miaka sita.

Amesema, ushirikiano huo unaleta urahisi na uwazi katika mchakato mzima wa kupata gari, ambao wateja hawatalazimika tena kufuata mlolongo mrefu kwa sababu kila hatua ya mchakato utashughulikiwa na Exim pamoja na GF Trucks.

“Hii inamaanisha kuanzia upatikanaji wa mkopo, ukabidhi wa gari jipya yani ziro kilomita, usajili na hadi bima vyote vinaunganishwa katika mfumo mmoja, na kufanya mchakato wa umiliki gari kuwa rahisi, nafuu na wenye uwazi kwa wateja,”amesema.

Kwa upande wake , Mkurugenzi wa GF Automobile Mujtaba Karmali,ushirikiano huo ni fursa ya kuwasaidia Watanzania wanaotamani kumiliki magari lakini wanakwamishwa na changamoto za gharama za awali.

“Kupitia ushirikiano thabiti tumeweza kuwaletea wateja wetu bidhaa bora kupitia huduma ya mikopo kutoka Exim, tunafanya umiliki wa gari kuwa jambo la kweli kwa Watanzania wengi zaidi na kuchochea ukuaji wa uchumi,”.

Mbali na wateja binafsi, mpango huu utawezesha pia wafanyabiashara wadogo,wa kati pamoja na kampuni kubwa kupata magari ya kuendesha shughuli zao bila kuathiri biashara hizo. Kwa kuwezesha upatikanaji rahisi wa magari.