Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online-Dar
BENKI ya Exim Tanzania imezindua kampeni yake ya miezi miwili ya matumizi ya kadi msimu wa sikukuu, iitwayo ‘Chanja kijanja, dili ndio hili.’ ambayo ilianza Desemba mosi 2025 na kumalizika Januari 31, 2026.
Kampeni hiyo inayolenga kuhamasisha wateja kutumia malipo yasiyotumia fedha taslimu na kuwazawadia wale wanaotumia kadi za Exim Mastercard kupitia mashine za POS na mifumo ya malipo mtandaoni katika kipindi cha ongezeko la matumizi ya ununuzi wa sikukuu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo,Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Exim, Andrew Lyimo, amesema, kampeni hiyo inaonesha dhamira ya benki kutoa huduma rahisi na salama kwa wateja wanaotumia mifumo ya malipo ya kidijitali.

“Kupitia kampeni hiyo tunataka kufanya malipo ya kila siku kuwa rahisi zaidi huku tukiwapa wateja fursa ya kushinda zawadi mbalimbali katika msimu huu wa sikukuu. Mpango huu unaaksi kujitoa kwetu, kukuza utamaduni wa malipo ya kidigitali na kuboresha uzoefu wa wateja kote nchini,” amesema Lyimo.
Pia amesema, kila wiki wateja watano wanajishindia zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu shilingi 100,000 kila mmoja, wateja 10 kushinda kiasi cha shilingi 200,000 pia wapo wanaorejeshewa fedha zao kulingana na miamala wanayofanya ikiwemo itakayofanywa sikukuu ya Christmas na zawadi kubwa kwa washindi mwishoni mwa kampeni ikitajwa kuanzia milioni 5 hadi milioni 15.
Aidha akizungumzia umuhimu wa kampeni katika kuendeleza matumizi ya malipo ya kidijitali, Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala na Mabadiliko ya Kidijitali wa Benki ya Exim Silas Mtoi, amesema kampeni hiyo ni zaidi ya zawadi , inalenga kubadili namna Watanzania wanavyopata uzoefu wa malipo ya kidijitali.
“Tunataka wateja wajisikie urahisi, kasi na usalama wa kutumia kadi kila wanapolipa, iwe dukani au mtandaoni, kwa kuongeza matumizi ya kadi, tunachochea safari ya kuelekea uchumi usio na utegemezi wa fedha taslimu na kuwawezesha wateja kufanya miamala ya kidijitali na yenye usalama zaidi. Hii si kampeni ya msimu huu pekee ni hatua ya kuelekea Tanzania yenye kujiamini kidijitali,”amesema Mtoi.

Nae Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim,Stanley Kafu, amesisitiza msimamo wa benki katika kuthamini wateja.
“Kampeni hii ni njia yetu ya kusherehekea na wateja msimu huu wa sikukuu,uwe unanunua mahitaji ya sikukuu, maandalizi ya sherehe za familia, safari za kwenda kuwatembelea wapendwa wako, kukata tiketi za mapumziko, kujaza mafuta kwa safari za barabarani, kufurahia chakula cha Krismasi na Mwaka Mpya, kununua vifaa vya sherehe, kulipia ada za shule kwa muhula ujao, au kufuatilia ofa za mtandaoni, kila ulipaji kwa kutumia kadi ya Exim unakupa urahisi, usalama, na nafasi zaidi ya kushinda msimu wote,”amesisitiza Kafu.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria