March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Exim benki kusogeza huduma Zanzibar

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online-Zanzibar

BENKI ya Exim kupanua wigo kwa kufungua tawi Zanzibar ili kusogeza huduma za kifedha karibu na watalii, wajasiriamali na jamii kwa ujumla kisiwani humo.

Hayo yamesemwa Februari 12,2026 na Ofisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim, Shani Kinswaga,amesema kufungulia kwa tawi jipya la Paje ni hatua ya kimkakati wa kupanua huduma za benki visiwani Zanzibar pamoja na kuimarisha mchango wake katika sekta ya utalii kama injini ya ukuaji wa uchumi.

“Tunaboresha ujumuishaji wa kifedha na kusaidia ukuaji endelevu wa uchumi unaotegemea utalii Zanzibar. Uwepo wetu visiwani umelenga kutoa huduma za kifedha zinazowezesha biashara kustawi na jamii kunufaika,”amesema Kinswaga.

Pia amesema benki hiyo imedhamini Z-Summit 2026 ikiwa kama mdhamini mkuu, hafla iliyoanza jana na kutarajiwa kumalizika leo kwenye Chuo Kikuu cha Zanzibar( SUZA).

Aidha imeelezwa kuwa, Z-Summit imejipatia umaarufu kama jukwaa kuu la biashara na uwekezaji katika utalii Zanzibar, ikiwakutanisha wawekezaji wa utalii, waendeshaji wawatalii, wamiliki wa hoteli na wengine.

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI), Suleiman Mohammed, ameipongeza Benki ya Exim kwa kuendelea kushirikiana na sekta ya utalii huku akisisitiza umuhimu wa msaada sa kifedha kwa ustawi wa sekta.

“Msaada wa kifedha ni muhimu kwa uendelevu wa sekta ya utalii. Dhamira ya Benki ya Exim na mipango yake ya kupanua huduma Zanzibar itasaidia kuongeza imani kwa wawekezaji na waendeshaji wa utalii,”amesema Mohammed.