Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) Mhandisi Modestus Lumato, amezitaka Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini kuhakikisha zinatoa taarifa sahihi za huduma ya maji na usafi wa mazingira kwa wananchi ili kushamirisha upatikanaji wa huduma endelevu kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Mhandisi Lumato ametoa maelekezo hayo leo Novemba 14,2022 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha Watendaji wa Mamlaka za Maji za Mikoa na Miradi ya Kitaifa kilicholenga kuhakiki taarifa za utendaji wa mamlaka hizo kwa mwaka 2021/22.
Mhandisi Lumato ameeleza kuwa tathmini iliyofanywa na EWURA imebaini kuwapo mamlaka za maji ambazo zimeendelea kuwasilisha taarifa zenye mapungufu kwenye kukidhi viwango vya huduma, uchakavu, ufanisi wa makusanyo wa maduhuli, muda wa upatikanaji wa huduma, ubora wa maji pamoja na idadi ya wananchi wanaopata huduma, hali hii inakwamisha kufanya tathmini ya hali halisi ya utendaji na upatikanaji huduma.
“Nitoe wito kwa mamlaka zote za maji kuhakikisha zinafanya masahihisho kwenye taarifa zenye mapungufu ili ziweze kutoa hali halisi ambayo mwisho wa siku itasaidia katika kupima utendaji na ufanisi wa huduma wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira” amefafanua Mhandisi Lumato
Kwa upande wake Mwakilishi wa katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Adam Ishara,amezitaka Mamlaka hizo kujitahidi kutekeleza wajibu wake kwa kutoa takwimu sahihi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa huku akisisitiza kuwa, Wizara ipo tayari kutoa miongozo na ushirikiano unaohitajika muda wowote.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira,ambaye ni Meneja Ufundi wa Maji na Usafi wa Mazingaira EWURA, Mhandisi Titus Safari,amesema kuwa mchakato wa maandalizi ya ripoti ya utendaji wa mamlaka za maji ni shirikishi hivyo kila mamlaka itumie kikao hicho kuthibitisha usahihi wa taarifa zake.
Watendaji kutoka Mamlaka 25 za Majisafi na Usafi wa Mazingira za miji mikuu ya mikoa na mamlaka 7 za miradi ya kitaifa wamehudhuria kikao kazi hicho kinachofanyika makao makuu ya EWURA jijini Dodoma.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote