November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yatoa leseni kwa wakandarasi wa umeme zaidi ya 300

Judith Ferdinand,Timesmajira Online, Mwanza

Katika kipindi cha miezi mitatu Julai-Septemba mwaka 2023 zaidi ya wakandarasi wa umeme(mafundi umeme) 300 walipatiwa leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA).

Huku ikielezwa kuwa mwitikio umekuwa mkubwa wa uwekezaji wa vituo vya mafuta vijijini katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa George Mhina Oktoba 18,2023 akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea ofisini kwake kwa ajili ya kueleza mipango na shughuli za taasisi hiyo ikiwa ni wiki ya wadau wa habari kutembelewa na waandishi wa habari ambao ni wananchama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC).

Ambapo ikiwa ni maandalizi ya kuelekea katika hafla ya usiku wa wadau wa habari Kanda ya Ziwa na waandishi wa habari iliondaliwa na MPC kwa udhamini wa wadau mbalimbali itakayofanyika Oktoba 20,2023 jijini Mwanza.

Mhina ameeleza kuwa idadi ya wakandarasi wa umeme kupatiwa leseni na EWURA kwa mwaka huu imeongezeka ukilinganisha na mwaka jana huku sababu kubwa ni kutokana na mamlaka hiyo kujikita katika kutoa elimu ya umuhimu wa leseni kwa mafundi hao.

Ambapo kati ya wakandarasi hao 375 waliopatiwa leseni kutoka Kanda zote nchini 84 ni kutoka Kanda ya Ziwa huku akiwasisitiza wananchi kutumia wakandarasi wa umeme wenye leseni kutoka EWURA.

Ameeleza kuwa mbali na elimu pia Shirika la Nishati ya Umeme Nchini(Tanesco), wameweka utaratibu katika huduma ya kuunganishwa nishati hiyo kuwa Mkandarasi wa umeme ambaye hana leseni kutoka EWURA hawezi kupeleka maombi ya mteja wake kwa ajili ya huduma hiyo ya umeme katika shirika hilo.

“Unapojaza fomu ya kuunganishiwa huduma ya umeme na Tanesco lazima uweke namba ya leseni ya Mkandarasi wako wa umeme ambayo imetolewa na EWURA,kwa sasa shirika hilo limeboresha mfumo wao vishoka kwa sasa hawana nafasi ya kufanya huduma bila ya kuwa na leseni kutoka kwetu hivyo kumefanya kuwa na muitikio mkubwa wa wakandarasi hao kupata leseni pamoja na kutoa elimu sana,” ameeleza Mhina.

Pia ameeleza sababu nyingine iliosaidia wakandarasi hao kujisajili na kupata leseni ni pamoja na EWURA kuboresha mfumo wa uombaji wa leseni hizo ambao wanaiomba kwa njia ya mtandao(online) na hata leseni anaipata kwa njia hiyo.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa muitikio umekuwa wa kuridhisha na mkubwa wa uwekezaji katika vituo vya mafuta vijijini katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwani wamepokea maombi mengi.

“Tumefurahi Kanda ya Ziwa watu wengi wamejitokeza kuwekeza katika vituo vya mafuta vya vijijini ambavyo gharama zake ni nafuu ambapo kuomba maombi ni 50,000,leseni ni shilingi laki tano kwa miaka mitano sawa na kiasi cha laki moja kwa mwaka,tumepunguza vigezo vya ujenzi wa vituo hivyo vya mafuta vijijini ambapo ukiwa na milioni 50 unaweza kujenga kituo hicho kijijini,”ameeleza Mhina.