




Na Mwandishi Wetu-SINGIDA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetoa elimu ya uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua kwa wadau mbalimbali mkoani Singida, wakiwemo wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu, viongozi kutoka wilaya ya Singida pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC), leo tarehe 13 Machi 2026.
Akiwasilisha mada kuhusu uvunaji wa maji ya mvua, Mhandisi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa EWURA Kanda ya Kati, Saidi Mwangalo, alieleza mbinu mbalimbali za kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua ili yaweze kutumika kwa muda mrefu na bila kuharibika.
Alisema uvunaji wa maji ya mvua ni njia muhimu ya kuongeza upatikanaji wa maji, hususan wakati wa ukame au pale kunapotokea changamoto katika huduma ya maji. Alisisitiza kuwa mvua ni rasilimali inayopatikana bure, hivyo ni muhimu kutunza na kutumia kila tone la maji ipasavyo ili kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji.
Washiriki pia walipatiwa elimu na Ofisa Huduma kwa Wateja, Bw. Juma Singano, kuhusu utaratibu wa kushughulikia malalamiko na kutatua migogoro kati ya watoa huduma na wateja wa sekta zinazodhibitiwa na EWURA
Mada nyingine zilizowasilishwa ni pamoja na utaratibu wa utoaji vibali vya ujenzi wa vituo vya mafuta mijini na vijijini, iliyowasilishwa na Mhandisi wa Petroli Kanda ya Kati, Bi. Roselyne Mndeme, pamoja na matumizi sahihi na salama ya gesi ya kupikia majumbani, iliyowasilishwa na Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa EWURA, Bi. Tobietha Makafu.
Akitoa neno la shukrani baada ya semina hiyo, Mkurugenzi wa Chama cha PPD, Ramadhan Mrisho aliishukuru EWURA kwa kuwafikia wanachama wao kwa elimu hiyo muhimu.
Pia aliishauri EWURA kuendelea kutoa elimu kwa jamii, hususan katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji, ili wananchi waweze kutumia misimu ya mvua kuvuna na kuhifadhi maji kwa matumizi ya baadaye.

More Stories
Kamati ya Bunge yaridhishwa ujenzi kampasi ya Mzumbe
Mwanasheria Mkuu wa Serikali aapishwa kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama
Megawati 50 za Umeme Jua Kishapu zaikosha Kamati ya Bunge