*Yatumia wiki ya huduma kwa wateja kutoa elimu kwa wananchi
*Wananchi zaidi ya 200 watembelea banda la EWURA
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Mamlaka za maji pamoja na TANESCO,zimetakiwa kuzingatia mikataba ya huduma kwa wateja pamoja na maadili ya utumishi wa umma kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Hii ikiwa ni pamoja na kuzingatia katazo la kutowakatia wananchi maji siku za mwisho wa wiki(weekend days) pamoja na sikukuu.
Hayo yameelezwa Oktoba 10,2025 na Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA),Kanda ya Ziwa, George Mhina,katika Wiki ya Huduma kwa Wateja duniani kwenye banda walioweka chini ya jengo la PSSSF ambalo ndipo ofisi za mamlaka hiyo Kanda hiyo zilizopo jijini Mwanza,ambapo wametumia wiki hiyo kutoa elimu kwa wananchi.

Mhina amesema,kupitia sheria ya maji,umeme na EWURA,mamlaka hiyo imepewa mamlaka ya kusimamia mikataba ya huduma kwa wateja.
Kwamba kila mamlaka zote za maji pamoja na TANESCO,zinatakiwa kuwa na mkataba wa huduma kwa wateja,ambao unaelezea haki na wajibu wa mtoa huduma na mteja.
“Lakini kupitia sheria zetu utaona kuna vitu vingi ambavyo baadhi za mamlaka za maji na Tanesco hawazitekelezi, mfano tukizungumzia kumkatia mteja maji,Sheria pamoja na mkataba wa huduma kwa wateja,ina kataza mteja asikatiwe huduma siku za mwishoni mwa wiki(weekend) na siku za sikukuu ni marufuku,”amesema Mhina.
Mhina amesema,pia Sheria na mkataba wa huduma kwa wateja,inamtaka mtoa huduma aidha ni mamlaka ya maji au TANESCO,kunapokuwa na tatizo la huduma itakayoathiri idadi kubwa ya watu pengine ni mtaa au Wilaya,kwa zaidi ya saa sita basi anatakiwa awataarifu wateja wake.
Pia kuna makatazo mengine na wajibu ambao mamlaka hizi zinatakiwa kufanya mfano kumfungia mteja huduma ndani ya siku saba au siku 30 baada ya kuwa amefanya malipo.
“Lakini kinachotokea kwa masikitiko hata kupitia wiki hii ya huduma kwa wateja kwa orodha ya waliotutembelea katika banda letu ni zaidi ya 200,kati yao malalamiko mengi yameangukia kwenye upande wa huduma ya maji ikiwa ni zaidi ya asilimia 92,”amesema Mhina na kuongeza:
“Wengine wanasema wamelipia huduma lakini hawajaunganishwa kwa zaidi ya miezi mitatu huku wengine wamekatiwa huduma bila kupewa notisi.Pia tunajua kuna maeneo hapa Mwanza yanachangamoto ya maji,yanaweza yasitoke hata siku mbili au tatu,lakini mamlaka husika haziwajibiki na hazitoi notisi kwa wateja wao,”amesema.

Hata hivyo Mhina, amesisitiza kuwa kama wasimamizi,wanachukua jambo hilo kwa umakini na kuhakikisha mamlaka hizo kwanza zinatangaza kwa wateja wao mikataba ya huduma kwa wateja ili wananchi waweze kujua haki zao na kufahamu wajibu wao.
“Lakini pia tutapita kwa wananchi kuwaelezea hiyo mikataba ya huduma kwa wateja walionayo hawa watoa huduma wetu,ili wananchi wanapokosa huduma wajue wanachukua hatua gani ikiwa ni pamoja na kuwasilisha malalamiko EWURA kwa kigezo cha mamlaka husika imeshindwa kuzingatia na kutekeleza mkataba wake,”amesema Mhina.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina