June 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yajivunia Mafanikio ya Kidijitali katika Wiki ya Utumishi wa Umma

Na Joyce Kasiki – TimesMajira Online, Dodoma

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeweka bayana hatua kubwa zilizopigwa katika kuboresha huduma kwa kutumia mifumo ya kidijitali, ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika Maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 17,2025 Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, amesema taasisi hiyo imejikita katika kuhakikisha huduma zinazodhibitiwa zinapatikana kwa urahisi, uwazi na ufanisi kupitia teknolojia, ili kuendana na kasi ya dunia ya kidijitali na matarajio ya wananchi.

Almebainisha kuwa huduma za EWURA zinagusa moja kwa moja maisha ya kila Mtanzania, hivyo matumizi ya teknolojia katika kusimamia mafuta, maji, gesi asilia na umeme si hiari tena, bali ni hitaji la msingi katika kuhakikisha uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wakati.

“Tumejipanga kuhakikisha kuwa kila mwananchi, hata yule aliye mbali na ofisi zetu, anaweza kupata huduma kupitia mifumo ya kidijitali. Hii ni hatua ya mageuzi ambayo inalenga kupunguza gharama, muda na usumbufu kwa wateja wetu,” amesema Dkt. Andilile.

Alieleza kuwa EWURA imeanzisha mifumo ya leseni ya mtandaoni, usajili wa watoa huduma, pamoja na mfumo wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa njia ya kielektroniki, hatua ambayo imesaidia kuongeza ufanisi na kupunguza mwingiliano usio wa lazima.

Katika banda lao la maonyesho, EWURA imeweka maafisa wa kutosha wanaotoa elimu, huduma na kupokea mrejesho kutoka kwa wananchi kuhusu huduma zinazodhibitiwa. Dkt. Andilile alisema ushiriki huo unaimarisha mahusiano kati ya mamlaka na wananchi kwa kuweka misingi ya mawasiliano ya pande zote mbili.

“Mfumo wetu wa mawasiliano ya moja kwa moja umesaidia sana kupunguza ucheleweshaji wa majibu. Wananchi wanaweza kuwasiliana nasi kupitia simu, barua pepe, tovuti au mitandao ya kijamii – na wanapata mrejesho wa haraka,” ameongeza.

Dkt. Andilile amesisitiza kuwa EWURA itaendelea kuwekeza katika mifumo ya TEHAMA, si tu kwa lengo la kuboresha huduma, bali pia kama sehemu ya utekelezaji wa dira ya serikali ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.

Aidha, alisema kuwa mamlaka hiyo inahimiza taasisi zote zinazodhibitiwa kuingia mikataba ya huduma kwa wateja na kuweka taarifa hizo wazi kwa wananchi kupitia tovuti zao, ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufuatiliaji wa huduma zinazotolewa.

“Haki ya mwananchi kupata taarifa sahihi ni msingi wa demokrasia na uwajibikaji. Ndiyo maana tunasisitiza mikataba ya huduma iwe wazi na ipatikane kirahisi kwa umma,” alisema Dkt. Andilile, huku akiitaka jamii kujenga tabia ya kufuatilia haki zao.

Katika kuelezea dhamira ya EWURA kwa mwaka huu, Dkt. Andilile alibainisha kuwa taasisi hiyo imelenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa kutumia kila fursa, ikiwemo maonyesho, mikutano ya hadhara na kampeni za uhamasishaji wa moja kwa moja mitaani.

Alisema kwamba changamoto nyingi zinazowasilishwa na wananchi katika maonyesho hayo ni sehemu ya tathmini ya ubora wa huduma na hutumika kama msingi wa maboresho ya sera, kanuni na mifumo inayotumika katika sekta za maji na nishati.

“Mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi unatuthibitishia kuwa wapo tayari kushiriki katika maboresho ya huduma. Tunalichukulia jambo hili kwa uzito kwa sababu tunaamini ushirikishwaji wa umma ni chachu ya mafanikio ya taasisi yoyote ya serikali,” alifafanua.

Dkt. Andilile alitumia nafasi hiyo pia kuwashukuru wananchi kwa namna wanavyojitokeza kwa wingi katika banda la EWURA, akieleza kuwa hilo ni dalili ya kuongezeka kwa uelewa kuhusu kazi za taasisi hiyo na umuhimu wa huduma wanazotoa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, EWURA imeweka mkakati wa muda mrefu wa kuongeza matumizi ya data kubwa (Big Data) na akili bandia (AI) ili kusaidia kufanya maamuzi ya haraka na sahihi katika kusimamia sekta wanazozihudumia.

Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo pia yatawezesha EWURA kuwa na mifumo ya tahadhari ya mapema kuhusu changamoto au ulegevu katika utekelezaji wa huduma, hivyo kuzuia matatizo kabla hayajawa makubwa kwa wananchi.

Katika kuhitimisha mahojiano hayo, Dkt. Andilile alitoa wito kwa wananchi wote kutembelea banda la EWURA katika maonyesho hayo, kutumia fursa ya kupata huduma, kutoa maoni na kujifunza zaidi kuhusu haki na wajibu wao katika huduma za nishati na maji.

Alisema ushiriki wa EWURA katika Wiki ya Utumishi wa Umma si wa maonyesho tu bali ni sehemu ya uwajibikaji wa taasisi hiyo kwa umma, na kwamba watatumia kila fursa kufikia wananchi kwa njia zote zinazowezekana ili kujenga taifa lenye huduma bora kwa wote.

Kwa ujumla, alisisitiza kuwa EWURA itaendelea kuwa sehemu ya mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za umma, kwa kuzingatia uwazi, ufanisi na ubunifu wa kiteknolojia, ikiwa ni mchango wao katika kufikia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Taifa la Tanzania.