Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Katika kudhibiti uuzwaji holela wa mafuta katika madumu hususani maeneo ya vijiji serikali kupitia Mamlaka wa Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji(EWURA),imehimiza wafanyabiashara kutumika fursa iliopo kujenga vituo vya mafuta vijijini.
Hayo yamebainishwa na Meneja EWURA Kanda ya Ziwa George Mhina wakati akizungumza na baadhi ya watu waliofika katika banda lao kwenye maonesho ya wakulima ya Nane Nane Kanda ya Ziwa Magharibi kwa ajili ya kupata elimu ya masuala yanayohusu nishati anabainisha mpango wa ewura pamoja na serikali katika kurahisisha upatikanaji wa nishati hasa mafuta vijijini.
Mhina amesema ili kukabiliana na changamoto ya uuzwaji wa mafuta kwenye madumu na wakati mwingine yanapoteza ubora pia yanakuwa hatarishi katika mazingira EWURA ikaamua kuja na kanuni ambazo ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini wamerahisisha.
Mfano ili uweze kujenga kituo cha mjini cha mafuta mpaka uwe na hati kutoka Halmashauri au Jiji ambayo inaruhusu kujenga kituo vilevile uwe na kibali kutoka NEMC na masharti ya ubora lazima uwe na zenge yenye urefu fulani na paa bora ambapo hivyo vyote vinachukua miaka kuvipata.
“Sisi EWURA tumetengeneza kanuni na tumepunguza masharti ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini ambapo vituo vingi vya mafuta mjini vina masharti mengi na magumu wakati mwingine kwa wananchi wa kawaida si rahisi kuyafikia,”amesema Mhina na kuongeza kuwa
“Ili kuimarisha na kuhimiza ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini masharti yale tumeyapunguza mfano kijijini hatuhitaji uwe na hati bali mhutsari wa kijiji ambao kupata ni ndani ya siku mbili na hatuhitaji uwe na kibali cha NEMC bali barua ya Mkurugenzi ioneshe kuwa kituo hicho hakitakuwa na madhara kwa mazingira na ujenzi wake ni wa kawaida,”.
Amesema,wataalamu wao walikaa wakafanya uchambuzi na kubaini kuwa kiasi kisichozidi milioni 50 kinaweza kujenga kituo cha mafuta kijijini kikawa na pampu mbili ya diezeli na petroli pia mifumo imerahisishwa na mambo mengine ambayo waliona yana urasimu wamerahisha kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo ameeleza kuwa Serikali katika kuunga jitihada za EWURA kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imetenga bajeti kwa mwaka jana na huu wa fedha ambapo inakusudia kukopesha wananchi kuweza kumudu vigezo na masharti vilivyo ainishwa kwenye muongozo, ambapo anaweza kukopeshwa Mtanzania hadi milioni 50 na ukajenga kituo cha mafuta kijijini.
Hivyo Mhina ametoa rai kwa wananchi na wafanyabiashara wa Kanda ya Ziwa watumie fursa iliopo ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini ili wananchi waepuke kununua mafuta kwenye vidumu na kuepuka hatari na majanga ambayo yanaweza kujitokeza kwa kuhifadhi mafuta kwenye madumu.
“EWURA pamoja na majukumu yetu sheria inatutaka kutoa elimu kwa umma,hivyo kutokana na maonesho haya tumeona ni eneo moja wapo la kufikisha elimu ya udhibiti kwa wanaMwanza na Kanda ya Ziwa kwa mwaka huu pamoja na kutoa elimu pia kuhimiza wananchi kuhusu fursa za ujenzi wa vituo vya mafuta rahisi na rafiki vijijini,”amesema Mhina.
Kuhusu nishati ya umeme Mhina,amewataka mafundi waliohitimu mafunzo ya umeme kuhakikisha wanafika EWURA ili kupata leseni na kutambulika kisheria ili kusaidia wananchi wanaotumia vishoka kuunganishiwa umeme kupata huduma hiyo kwa urahisi.
“Tunahimiza kuwa kwa sasa majanga ya moto yamekuwa yakiongezeka wananchi wametakiwa kutumia mafundi umeme waliopata leseni kutoka EWURA takwimu mpaka sasa nchi nzima kuna mafundi 5000 waliopata leseni na Kanda ya Ziwa wapo 1200, tunawasisitiza mafundi waliopita Veta na kusomea ufundi wa umeme waje kwetu kuomba leseni na kuweza kutambulika kisheria,”amesema Mhina.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato