March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yahimiza uwekezaji ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini 

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Wadau mbalimbali Kanda ya Ziwa wamehimizwa kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini,ili kuwasogezea wananchi wa maeneo hayo huduma karibu na kuondokana na hatari ya uuzwaji na ununuaji wa nishati hiyo kwenye vidumu.

Ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji(EWURA), imesisitiza kuwa uwekezaji katika ujenzi wa vituo vya mafuta maeneo ya vijijini ni rahisi kwani gharama yake ni nafuu huku baadhi ya masharti yakipunguzwa yakilinganishwa na maeneo ya mjini.

Akizungumza  Agosti 3,2025,kwenye banda la mamlaka hiyo katika maonesho ya Wakulima Nane Nane,kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yanafanyika Nyamh’onglo wilayani Ilemela mkoani Mwanza,Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina,amesema,kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, nchi ilikuwa na vituo vya mafuta vijijini  279.

Lakini katika kipindi cha miaka minne vituo vya mafuta vijijini vimeongezeka na  kufikia 515 ikiwa ni  karibu vituo 300 vimeongezeka katika maeneo hayo ya vijijini.

Mhina ,amesema ongezeko hilo linatokana na kupunguzwa kwa masharti na gharama za ujenzi za vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini ambapo kwa kiasi cha milioni 50, mtu anaweza kufanya uwekezaji huo.

Huku akisisitiza  kuwa ujenzi wake ni rahisi ikilinganishwa na maeneo ya mjini akitolea mfano Wilaya ya Nyamagana au Ilemela jijini Mwanza ambapo uwekezaji wa kujenga kituo cha mafuta  kimoja ni gharama kwani mtu anaweza kutumia zaidi ya milioni 250.

“Sababu vituo vya mafuta mjini vina masharti mengi ambapo muwekezaji atahitajika kuwa na hati inayopatikana kwenye Halmashauri za Jiji au Manispaa na wakati mwingine inachukua muda kuipata na ni gharama.Pia muwekezaji  atapaswa kuwa na hati ya mazingira inayotolewa na NEMC,ambayo pia wakati mwingine kupata inaweza kuchukua muda na ni gharama,”amesema  Mhina na kuongeza:.

“Vituo vya mafuta mjini ukiangalia ujenzi wake kwa maana vigezo vyake vya kiufundi kwa maana ya sakafu  na paa,vinapaswa kujengwa kwa kuzingatia vigezo fulani  pia ni gharama kubwa,”.

Aidha amesema,kwa upande wa vijijini wamepunguza masharti moja wapo hawahitaji muwekezaji awe na hati miliki ya ardhi bali awapelekee mhutsari wa kijiji unaoonesha kuwa yeye ndiye mmiliki wa eneo hilo au amekodishwa na ndani ya siku moja anaweza kuupata.

Pia amesema, hawahitaji muwekezaji awe na kibali cha mazingira kutoka NEMC bali ni barua ambayo imesainiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri husika ikionesha kwamba kituo kipo kijijini na ujenzi wake hautaathiri mazingira.

“Tunajua wananchi wa Kanda ya Ziwa hususani wa Mwanza ni wafugaji na wakulima,

wakiuza ng’ombe zao watapata fedha na kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini,kwani masharti tumepunguza kwa milioni 50 atajenga kituo na kutoa huduma  kwa jamii,”amesema Mhina.