January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA, LATRA kudhibiti changamoto usafirishaji mafuta

Na Jackline Martin, TimesMajira Online, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), imeingia makubaliano na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) wenye lengo la kufanya kazi pamoja.

Hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto mbalimbali ikiwemo udhibiti wa mafuta na usafirishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa EWURA, Ahmad Kilima amesema EWURA na LATRA wanakazi moja ya kufanya.

Amesema EWURA wanaangalia ubora wa bidhaa yenyewe na wanadhibiti upande wa uchumi wa bidhaa ya mafuta.

“EWURA na LATRA wanakazi moja ya kufanya, sisi tunaangalia ubora wa bidhaa yenyewe na tunadhibiti upande wa uchumi wa bidhaa ya mafuta na wenzetu waangalia usafiri wa hiyo bidhaa ili iweze kumfikia mtumiaji katika hali inayokusudiwa,” amesema Kilima.

Amesema mkataba huo utakuwa ni chachu ya ushirikiano wa utekelezaji wa majukumu ya udhibiti na usimamizi wa miundombinu ya usafirishaji kwa pamoja ikijumuisha kufanya uamuzi wa pamoja, kuimarisha elimu kwa umma, usalama wa mzingira na kuangalia usalama wa watu na mali zao.

Ameongeza kuwa, LATRA kazi yao ni kuangalia usafiri wa hiyo bidhaa ili iweze kumfikia mtumiaji katika hali inayokusudiwa.

“Sisi EWURA tutajitahidi kuhakikisha ubora wa bidhaa ambazo zinasafirishwa mahali popote,” amesema Kilima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa LATRA, Godfrey Chibulunje amesema kwa hatua waliofikia jana ya kusaini mkataba wa kufanya kazi pamoja utasaidia kuondoa changamoto zilizopo katika usafirishaji wa bidhaa ya mafuta

“Siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya malori kuanguka na kushika moto na wananchi kukimbilia kupata mafuta na tumeona athari kutokana na vitendo hivyo, lakini kupitia makubalaino yetu yatasaidia kuaondoa hali hiyo,” ameesema Chibulunje.