Na Penina Malundo, Timesmajira
Kwa mara ya pili, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeshinda tena tuzo ya Uhusiano Mwema na Vyombo vya habari nchini, kwa mwaka 2024 ikidhihirisha namna taasisi hiyo inavyothamini ushirikano na uhuru wa vyombo vya habari katika kuuhabarisha umma kuhusu shughuli za udhibiti wa huduma za nishati na maji.
Tuzo hiyo iliyotolewa jana Machi 29,2025 na Chama cha Maofisa Uhusiano Tanzania (PRST), baada ya mchuano mkali uliohusisha taasisi nyingi imeipa EWURA heshima na ari ya kuendelea kudumisha uhusiano wake thabiti na vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari nchini.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo amesema ushindi huo kwa mara ya pili mfululizo ni kielelezo cha utawala bora, uwazi, uwajibikaji, na miongozo inayotolewa na Bodi na Menejimenti ya EWURA, chini ya mwemyekiti wake Prof. Mark Mwandosya na Mkurugenzi wake Mkuu, Dkt. James Mwainyekule.
Vigezo vilivyotumika kuipatia EWURA ushindi huo ni kuwa na mpango mkakati bora wa ushirikishwaji wa vyombo vya habari, ubora wa maudhui na uthabiti wa utoaji taarifa pamoja na mtazamo walionao vyombo vya habari kuhusu Mamlaka hiyo.
Wakati huo huo, Janeth Mesomampya, ambaye ni Ofisa Uhusiano wa EWURA amepokea tuzo ya Ofisa Uhusiano bora kwa mwaka 2024, akiwa mmoja wa washindi watano katika kipengele hicho.
Rais wa PRST Assah Mwambene, amesema utoaji wa tuzo hizo ni chachu kwa wataalam walioko kwenye kada hiyo kufanya kazi zao kwa ubora zaidi ili kuimarisha huduma katika maeneo yao ya utendaji.
EWURA ilipata tuzo ya aina hiyo pia kwa mwaka 2022, iliyotolewa na PRST kutambua mchango wake katika kushirikiana vyema na vyombo vya habari nchini.
More Stories
Vijana watahadharishwa kuelekea uchaguzi mkuu
Mkandarasi atakiwa kujenga haraka daraja la muda Bonyokwa
Rais Samia asisitiza amani nchini