January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA CCC yawapiga msasa wahudumu wa afya ngazi ya jamii Musoma

Na Fresha Kinasa,TimesMajira Online ,Mara

BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA CCC) Mkoa wa Mara limeendesha semina kwa Wahudumu wa Afya ya Msingi ngazi ya Jamii Katika Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara, kwa lengo la kuwajengea uelewa mpana kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwemo haki na wajibu wa Watumiaji wa nishati, pamoja na watoa huduma ili kuendelea kuimarisha Mlmahusiano bora baina ya pande zote.

Semina hiyo imefanyika Oktoba 16, mwaka huu, katika Ukumbi Mkoa wa Mara, na kuwahusisha watoa huduma wa nishati ikiwemo maji, gesi, umeme, ambapo Mwenyekiti wa Baraza hilo Mkoa wa Mara Robinson Wangaso, amesema Baraza hilo limekuwa na utaratibu wa kukutana na Watoa huduma na watumiaji kutoka makundi mbalimbali ikiwemo wajasiriamali, wafanyakazi, wahudumu wa afya, na wananchi kwa lengo la kuwapa elimu ikiwa ni utekelezaji wa majukumu ya baraza hilo kwa mujibu wa sheria.

Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati Mkoa wa Mara Robinson Wangaso akitoa semina kwa Wahudumu wa Afya ya Msingi ngazi ya Jamii wa Manispaa ya Musoma.Kulia kwake ni Kaimu Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MUWASA)Chausiku Joseph

Akizungumza matika semina hiyo, Wangaso amesema kuwa EWURA CCC inawajibu wa kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa maji na nishati kama ilivyo dhamira ya kuanzishwa kwake, sanjari na kuhakikisha inapokea malalamiko na kero mbalimbali za watumiaji wa huduma za nishati na maji na kuweza kuzipatia ufumbuzi kwa maslahi mapana ya pande zote mbili yaani watumiaji na watoa huduma.

“Ni wajibu wa mtumiaji wa huduma iwapo ana kero kuziwasilisha kwenye Baraza la ‘EWURA CCC’ kwa njia ya maandishi ambapo tutaita pande zote mbili na kufanya usuruhishi, ili kila pande ipate haki lengo ni kuwezesha mtumiaji kupata huduma bora na mtoa huduma kupata manufaa kutokana na ubora wa huduma yake anayoitoa, niseme kuwa,mtu anapokuwa na kero cha kwanza amweleze mtoa huduma ikishindikana alete malalamiko yake ‘EWURA CCC’ na siyo kwenda Polisi ama sehemu nyingine lengo kupata usuruhishi wenye tija” amesema Wangaso.

Wahudumu was afya ya Msingi ngazi ya Jamii wa Manispaa ya Musoma wakiwa kwenye semina ya kuwajengea uelewa iliyoendeshwa na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati ‘EWURA CCC’ Mkoa wa Mara. Picha zote na Fresha Kinasa

Naye Winfrida Bihemo Mjumbe wa ‘EWURA CCC’ Mkoa wa Mara akitoa mada Katika semina hiyo, kuhusiana na ufahamu juu ya haki na Wajibu wa mtumiaji wa huduma amesema kuwa, mtumiaji wa huduma za nishati na maji anahaki ya kuelimishwa, haki ya kufidiwa iwapo amepata hasara kutoka na huduma aliyotumia, kulalamikia huduma iwapo haikidhi ubora, kupewa mwongozo wa utatuzi migogoro.

Pia Bihemo ameongeza kuwa, mtumiaji wa huduma anawajibu kulipia ankara ya huduma aliyopewa kwa wakati, kutunza miundombinu ya huduma iweze kuwa endelevu, kutoa taarifa akigundua bidhaa anayotumia iwapo inakasoro, pamoja na kufuata taratibu na makubaliano ya mkataba wa huduma wakati wote bila kukiuka.

Kwa upande wake Afisa Msaidizi Utawala na Huduma kwa Wateja ‘EWURA CCC’ Mkoa wa Mara Denis akiwasilisha mada kuhusiana na kanuni za Ubora wa huduma za maji na Usafi wa Mazingira amesema kuwa, kwa mujibu wa kanuni ya 16 (1) ukaguzi na upimaji wa mita unapaswa ufanyike mteja akiwepo eneo huska ili kuondoa malalamiko, huku pia akisisitiza kuwa mteja akikatiwa huduma kimakosa ikiwemo maji atakuwa na haki ya kulipwa fidia kwa mujibi wa kanuni ya 29 (1) sambamba na kurejeshewa huduma ndani ya Saa 24 iwapo mteja atalipa deni lililopelekea akatiwe huduma kwa mujibu wa kanuni ya 31( 1).

“Utaratibu wa kulipa ankara kwa mujibu wa kanuni ya 23 (1) mteja anatakiwa kulipa ankara yake ndani ya siku 30 kutokea pale alipopokea ankara yake Kama hatakuwa na uwezo ni wajibu wake kufika sehemu huska na kutoa taarifa, tunahitaji elimu hii iwafikie Wananchi wote kusudi watambue wanapolipia kwa wakati huduma inamsaidia mtoa huduma kupanua wigo wa huduma yake kwa watu wengine tena.” amesema Danu.

Erasto Kisha kutoka Makao makuu ya ‘EWURA CCC’ Jijini Dar es laam amewataka waliohudhuria mafunzo hayo kuhakikisha wanakwenda kuyatumia kwa faida ikiwemo kuwaelimisha wengine ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria, huku akibainisha kuwa wamejipanga vyema kupeleka elimu hiyo mpaka ngazi ya chini maeneo mbalimbali Nchini.

Kwa upande wao washiriki wa semina hiyo, Christina Elias na Ester Juma Wakazi wa Manispaa ya Musoma wakizungumza kwa nyakati tofauti Wamesema elimu waliyoipata imewafungua, kwani mambo mengi hawakuweza kuyajua kabla ya semina hiyo, ambapo wamesema wamepata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali na kupewa majibu kutoka kwa Watoa huduma na nishati na Maji na pi wameahidi kwenda kuwa mabalozi wema wa kuwaelimisha Wananchi wengine Katika majukumu yao.