December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EU yasisitiza msimamo wake vita ya Ukraine

Na David John

UMOJA wa Ulaya nchini umesema unasimama na Ukraine kuhakikisha vita baina ya Ukraine na Urusi inamalizika kwa njia ya mazungumzo ili kuepuka madhara zaidi yanayoweza kujitokeza

Hayo yalisemwa Mkoani Dar es Salaam jana na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzaia, Nabil Hajloui pamoja na mabalozi wengine wakiongozwa na Balozi Manfredo Fanti walioko nchini ambao nchi zao ziko kwenye Umoja wa Ulaya( EU.)

Akitoa taarifa ya Ufaransa na Umoja wa Ulaya ,Balozi Nabil Hajloui alisema Machi 2,2022 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio ambalo linaitaka Urusi kusitisha mara moja matumizi ya nguvu dhidi ya Ukraine katika kura iliyoidhinishwa kwa wingi na nchi 141 ikiwa ni pamoja na nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya huku nchi tano zikipinga na nchi 35 kuacha kupiga kura Kati ya wanachama 193 wa Jumuiya.

Aliongeza kuwa Ufaransa na Umoja wa Ulaya zilijiunga karibu na Jumuiya zima ya Kimataifa katika kulaani vikali mashambulizi ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine anbapo ni shambulio kubwa zaidi juu ya Usalama wa Ulaya katika miongo kadhaa.

“Kukabiliwa na vita vilivyoanzishwa na Urusi bila uchokozi wowote na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa na ahadi zake zote,nchi 27 wanachama wa EU zimepitisha vikwazo vikubwa dhidi ya Urusi.

Jumuiya inasikitisha na matumizi makubwa ya nguvu yanayotumika kuishambulia Ukraine,”alisema wakati akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari akiwa na viongozi kadhaa wa Umoja wa Ulaya.

Alisema kuwa EU imeamua kuweka vikwazo vya moja kwa moja kwa watu wanaohusika na maamuzi yanayohusiana na vita lakini pia mfumo wa kiuchumi wa umma na wa kibinafsi wa Urusi ambao unaunga mkono juhudi hizo za vita na kwamba katika upande wa kifedha Urusi iko karibu kuondolewa kwenye masoko ya kifedha.

“Vikwazo hivyo pia vitakuwepo katika kuzuia Uwekezaji wote katika sekta ya nishati ya Urusi na utangazaji wa vyombo vya habari ambavyo vinarudisha propaganda za vita vya Urusi katika EU. Tayari vikwazo hivyo vimeanza kufanya kazi,”ameongeza Balozi Nabil .

Pia alisema EU iko tayari kuongeza shinikizo zaidi ili kuongeza ukali wa vita kwa Urusi ili kuifanya nchini hiyo kuamua kusitisha mapigano na kufikia mazungumzo kama Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alivyotangaza katika mkutano wa wakuu wa nchi za Ulaya wa Versailles Machi 10-11 mwaka huu.

Katika taarifa ya Ufaransa na Umoja wa Ulaya inaeleza wanachama wa EU wanaunga mkono ufunguzi wa uchunguzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai katika mashambulizi y Urusi na kisababisha majeruhi ya raia.Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliamuaru Urusi kusitisha uvamizi nchini Ukraine.” Hata hivyo Rais Emmanuel Macron anaendelea na mazungumzo na Vladimir Putin ili kupata suluhisho la amani katika mgogoro huo.

Wakati huo huo Balozi Nabil pamoja na EU wametoa ombi kwa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kutoa kauli kwa Urusi ili iwezeshe kusitisha vita dhidi ya Ukraine na kwamba nchi za Afrika zinatambua madhara yanayopatikana kutokana na vita hiyo.

Viongozi hao wa Umoja wa Ulaya wameeleza kuna maelfu ya raia kutoka Mataifa mbalimbali wamelazimika kukimbia makazi yao na wengine kuacha shughuli zao na miongoni mwao wamo walioacha masomo kwasababu ya vita inayoendelea Ukraine.