Na Penina Malundo, TimesMajira Online
UMOJA wa Ulaya (EU) kupitia mradi wa upembuzi yakinifu wa miundombinu ya kusafirisha na kupoza umeme umeandaa mafunzo ya siku nne kwa wataalam 25 kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC).
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo yanayofanyika kwa njia ya video hayo yaliyoanza Julai 27 hadi 30,202, Mkufunzi Mkuu na Meneja Mradi wa Kampuni ya Studio Pitrangeli ya nchini Italia, Stefano Galantino amesema mafunzo hayo yanatoa fursa kwa wataalam hao kuongeza uwezo na ujuzi katika kusanifu miradi ya njia za umeme wa msongo mkubwa.
Amesema lengo la mafunzo ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo na ujuzi wa kusanifu na kusimamia ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa na vituo vya usambazaji na upozaji wa umeme.
“Kupitia mafunzo haya ambayop tunawajengea uwezo yataweza kuwapa fursa wataalamu hawa kutathimini na kusanifu miradi ya kusafirisha umeme hususani katika maeneo ya vijijini,”amesema
Kaimu Meneja wa Mipango Miradi na Utafiti wa REA, Mhandisi Jensen Mahavile amesema mafunzo hayo yatawapa fursa ya kuongeza ujuzi katika kutathmini na kusanifu miundombinu ya kusafirisha na kupoza umeme.
Amesema kwa zaidi ya muongo mmoja EU imekuwa ukishirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha na kuongeza upatikanaji huduma ya umeme kwa kufadhili miradi mbalimbali ya umeme, matumizi bora ya nishati, nishati jadidifu na nishati bora ya kupikia.
Mahavile amesema mradi huu wa Upembuzi Yakinifu wa Njia za Umeme wa Msongo Mkubwa na Vituo vya Usambazaji na Upozaji wa Umeme ni wa kimkakati wenye kuwezesha kupanga na kutekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini kwa kuongeza wigo wa mtandao wa gridi ya Taifa.
Awali mafunzo haya yalipangwa kufanyika mjini Rome nchini Italia zilipo ofisi za Mshauri Muelekezi hata hivyo kutokana janga la ugonjwa wa Korona yamefanyika nchini kwa njia ya video.
Mada zilizotolewa ni miundombinu ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa, tathimini ya vituo vya kupoza na kusambaza umeme, kusanifu miundombinu hiyo pamojana na tathimini ya uchumi na fedha katika mradi huo.
More Stories
TARURA Kilimanjaro yatimiza ahadi ya Rais Samia
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime