Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa jamii bado inahitaji elimu juu ya masuala yanayohusu usawa wa kijinsia pamoja na ushiriki wa wanawake na wasichana katika shughuli za kiuchumi ili kufikia malengo ya agenda ya 2030 ya maendeleo endelevu.
Kwa kutambua uhitaji huo kupitia mradi wa miaka 7,(2021-2028),wa Uwezeshaji kupitia ujuzi (ESP)unaotekelezwa na vyuo na taasisi za Canada(CICan) kwa ushirikiano wa karibu na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia ya Tanzania kupitia Idara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi(DTVET) kwa ufadhili wa serikali ya Canada inatoa mafunzo ya siku tano kwa wakufunzi(ToT), ya kuwajengea uwezo katika kazi zao za mbalimbali ikiwemo ya kukuza usawa wa kijinsia yanayofanyika jijini Mwanza.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mshauri wa Masuala ya Kijinsia kutoka CICan,Dkt.Alice Mumbi, ameeleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuzijengea uwezo asasi za kijamii(Cabos), vyuo ya maendeleo ya wananchi,Idara ya maendeleo e jamii na Wizara ya Elimu,ili ziweze kutoa semina na mafunzo mbalimbali pamoja na kampeni kuhusu masuala ya usawa wa kijinsia,haki za binadamu kwa makundi katika jamii na taasisi zao.
Dkt.Alice ameeleza kuwa pia kupitia mafunzo hayo washiriki watapewa mbinu mbalimbali na zana zitakazowasaidia katika utekelezaji wa majukumu ya mradi kwenye jamii na taasisi zao.
“Lengo kuu la mradi ni kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika shughuli za kiuchumi, tunaamini jamii ikihamasishwa na kupewa elimu hii,tutapata mabadiliko chanya yatakayowezesha kundi hilo kupata ujuzi wa fani mbalimbali na ujasiriamali kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi na asasi za kijamii,”ameeleza Dkt.Alice.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa lengo la mradi ni kuona kwamba kuna ufahamu na uelewa zaidi kuhusu usawa wa kijinsia na haki za binadamu pamoja na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa mtoto wa kike wa kupata nafasi sawa ikiwemo elimu,ushiriki wa kiuchumi na kupata haki za binadamu.
Dkt.Alice ameeleza kuwa wanalenga pia kufanya kazi kwa kuhakikisha vyuo vya maendeleo ya jamii vimewezeshwa kutoa fani tofauti tofauti za kuwawezesha watoto wa kike kupata kipato chao kupitia ujuzi ikiwemo kufanya ujasiriamali,kuajiriwa au kujiajiri.
“Tunatazamia zaidi ya walengwa 5000 watanufaika na mradi huu kwa kupata nafasi ya mafunzo katika fani mbalimbali za muda mfupi wa ikiwemo wiki moja au mbili na miezi mitatu hadi mwaka pamoja na kupata mitaji ya kuanzisha ujasiriamali,”ameeleza Dkt Alice.
Kwa upande wake Mkufunzi Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,Gloria Mrifoel, ameeleza kuwa Mradi huo pia umekuja na mtazamo mwingine wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia.
Ambapo kwenye jamii bado kuna tatizo kwani unakuta mtoto wa kike amekatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali hivyo lazima kuelimishana kama jamii itambue haki ya mtoto wa kike ni haki ya binadamu.
“Lazima wawepo watu wenye uelewa wa kufahamu masuala ya usawa wa kijinsia ambao watakwenda kupeleka ujumbe kwenye jamii zetu kwa, kuhamasisha,kuelimisha na kueleza umuhimu wa binadamu wa jinsi zote na katika kuwezesha kupata fursa sawa katika mambo mbalimbali na kupunguza mwanya uliopo wa utekelezaji wa majukumu kati ya mwanamke na mwanaume,hivyo washiriki muelewe kwamba mnadhamana ya kupeleka ujumbe kwa jamii kwa ajili ya maendeleo endelevu ya taifa,”ameeleza Gloria.
Naye Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Kasulu Gabriel Milombetse, ameeleza kuwa funzo hayo ni muhimu kwa sababu wanapotoka wanasimamia jamii ambayo kimsingi inakumbwa na masuala yanayohusu haki za binadamu hususani wanawake na watoto wa kike wanakosa haki zao za msingi ikiwemo kukatisha masomo.
“Masuala ya usawa wa kijinsia tunaona tunapotoka jamii kubwa wanawake na watoto wa kike hawapati stahiki zao kulingana na mazingira halisi yaliopo kwenye jamii mafunzo haya yatatujengea uwezo mzuri ambao tutaenda kuisaidia jamii ambayo inatuzunguka,”ameeleza Gabriel.
More Stories
Wasanii wa ‘Comedy’ kuwania tuzo
Wazazi wa Wanafunzi Sekondari ya Muhoji waamua kutoa chakula kwa watoto wao
Jokate achangia milioni 3 mfuko wa bodaboda