December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EMEDO,yahimizwa kuongeza kasi elimu ya usalama majini.

Fresha Kinasa, TimesMajira Online Musoma.

MKUU wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi,amelihimiza Shirika lisilo la Kiserikali linalotekeleza mradi wa ‘kuzuia kuzama Ziwa Victoria’ la Environment and Economic Development Organization (EMEDO),kuwafikia wananchi wengi zaidi mkoani humo,kwa ajili ya kuwapa elimu ya usalama majini.

Kanali Mtambi, ameyasema hayo Septemba 26, 2024,alipotembelea banda la EMEDO,kilele cha maadhimisho ya siku ya usafiri wa maji duniani na miaka 50 ya Uanachama wa shirika la Bahari duniani, yaliyofanyika kitaifa kuanzia Septemba 23, 2024 hadi Septemba 26, 2024, Mjini Musoma.

Kanali Mtambi,amesema, Mkoa wa huo umezungukwa na Ziwa Victoria,na Wananchi wanatumia usafiri wa majini. Hivyo, ili waendelee kuwa salama shirika hilo linalojukumu la kuendelea kutoa elimu, kwa wavuvi na wananchi wanaotumia vyombo vya usafiri wa majini kutumia makoti okozi na kufuata sheria.

“Ongezeni kasi ya utoaji wa elimu ya usalama majini, ili iwafikie wananchi wengi zaidi.Tutaondokana na ajali za majini iwapo wananchi watakuwa na elimu ya kutosha kuhusu usalama wao wanapotumia vyombo vya majini,”amesema Kanali Mtambi.

Kwa upande wake,Ofisa Mradi wa ‘Kuzuaia kuzama Ziwa Victoria’ Majura Maingu,amesema Shirika la (EMEDO) limetoa elimu ya usalama majini kwa muda wa miaka mitatu. Ambapo wavuvi na wananchi zaidi ya 9000 wa mialo ya Busekera na Kome katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma walifikiwa.

Maingu amesema, Mradi huo ulianza mwaka 2021 na unatekelezwa katika Halmashauri ya Musoma baada ya kufanyika utafiti na kutambua hatari zilizoko katika jamii zinazosababisha watu kuzama majini.

Ambazo ni ukosefu wa elimu ya usalama majini, vifaa vya kujiokolea, tabia ya baadhi ya Wavuvi na Wananchi kuingia majini wakiwa wamelewa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Maingu amesema, elimu hiyo imetolewa kwa Wavuvi na Wananchi, wamiliki wa vyombo vya majini, mafundi wa vyombo vya majini na pia wasimamizi wa sheria (BMU) na viongozi wa serikali katika maeneo hayo na imeleta manufaa makubwa.Kwani robo tatu ya wavuvi na wananchi katika mialo waliyotoa elimu wanavaa makoti okozi na kuzingatia sheria.

Pia amesema, EMEDO imekuwa ikishirikiana na Mamlaka zinazohusika na usalama majini wakiwemo Maafisa Uvuvi, TASAC, wanafunzi wa shule jirani na maeneo hayo, wanawake wanaofanya kazi kwenye mialo (wasomba ngese), TMA, Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, BMU pamoja na Wizara mtambuka zinazohisiana na usalama Majini.

Maingu ameongeza kuwa, kwa sasa wanatengeneza koti okozi kwa bei nafuu ambazo zinatumia chupa za maji (Local Life Jacket Ring) ambazo zitaanza kuuzwa kwa gharama ya Shilingi 8,000,ili wavuvi na wananchi waweze kuvaa wakati wote wawapo majini.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka, amewaomba wananchi waliopata elimu ya usalama majini,kuwa mabalozi kwa kuwaelimisha wengine na kuitumia elimu waliyoipata kwa vitendo ili iwe na manufaa.