November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Elimu zaidi itolewe kwa jamii kuondoa dhana potofu,mauaji ya watu wenye ualbino

Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza

Ili kukabiliana na changamaoto ya mauaji ya watu wenye ualbino nchini elimu inatakiwa kutolewa kwa jamii ili iondokane na dhana potofu ya kuwa kiungo cha watu hao kinaweza kuleta utajiri huku msisitizo ukitolewa kuwa utajiri unapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii.

Huku Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza pamoja na jamii husika kuhakikisha wanaimarisha ulinzi kwa watu wenye ualbino na kuchukua hatua kali dhidi ya wale wanohusika na vitendo vya ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kuua na kufanya vitendo vingine vya kikatili dhidi ya albino.

Akisoma risala Julai 15,2024 mbele ya mgeni rasmi wa mdahalo wa kukomesha mauaji ya watu wenye ualibino Mkoa wa Mwanza ulioenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya ‘’We ring the bell” ulioandaliwa na Chama cha watu wenye Ualbino(TAS),Mkoa wa Mwanza na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC),uliofanyika jijini hapa M jumbe wa TAs Mashaka Tuju,amesema wananchi wamekuwa na elimu ndogo juu ya watu wa kundi hilo.

“Kumekuwa na imani potofu kwa jamii juu ya watu wenye ualbino na kusadikika kuwa viungo vyao vinapopelekwa kwa waganga vinaleta bahati ya utajiri,hii ni dhana potofu ambayo ikiondolewa vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino vitaisha kwenye jamii,”ameeleza Tuju.

Pia ameeleza kuwa jambo jingine katika kukomesha mauaji hayo ni kushirikiana na MPC kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari mbalimbali vilivyopo mkoani Mwanza ili wananchi wapate uelewa juu ya ualbino nakuondoa imani potofu zinazopelekea mauaji ya watu wa kundi hilo.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Daniel Machunda amesema kuwa “Wanamwanza kataa kupotoshwa na waganga wapiga ramli chonganishi,unaambiwa kuwa ukalete kiungo cha mtu mwenye ualbino utakuwa tajiri,mbona albino mwenyewe siyo tajiri ambaye yeye ndio mwenye viungo.”Sasa imetosha mauaji ya Albino Mwanza,”.

Machunda ameeleza kuwa serikali ya Mkoa wa Mwanza haitakuwa na simile katika jambo hilo kwani ni vitendo vya aibu.

“Lazima tulaani vikali vitendo hivi vya kinyama ambavyo havitegemewi kufanywa au kutokea katika jamii yoyote ya watu waliostaarabika na wanao mwabudu Mungu,mauaji ya albino ni jambo linalofedhehesha na kuaibisha mkoa wetu ni vitendo visivyosimulika,hivyo hatuna budi sote kuhakikisha kuwa tunapambana kupinga ukatili na mauaji hayo kwa nguvu zote,”.

Mwenyekiti wa TAS Mkoa wa Mwanza Stalone Makoye ,ameeleza kuwa wameamua kuja na kampeni ya ‘We ring the bell'(kuliza kengere), lengo ikiwa ni kila mmoja katika jamii kutonyamazia vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya mtu mwenye ualbino.

“Kupitia kampeni hii kila mmoja akitoa elimu ,akaripoti tukio au viashiria ambavyo vinaweza kumsababishia mazingira mabaya mtu mwenye ualbino kwa kutoa taarifa ,tunaamini ushirikiano kuanzia jirani aliopo nyumbani ,mama na baba mzazi,wanafamilia wote, na ikianzia nyumbani kuliza kengere na jirani naye ataliza kengere,shuleni pia wataliza kengere,Diwani naye ataliza kengere hivyo jamii nzima italiza kengere na itafikia kuwa mauaji haya yatakuwa fikra hafifu za kihistoria ambazo zimepitwa na wakati na mauaji yatatoweka katika nchi yetu,”.

“Ukiona mtu anamfanyia ukatili mtu mwenye ualbino wewe ukasimama kati ukasema upasi kumfanyia hivi kwani nay eye ni binadamu kama wengine hapo utakuwa umeliza kengere,,jirani nyumbani kuna mtoto mwenye ualbino hawampeleki shule kwa sababu ya ulemavu wake ,wewe ukasema hapa anatakiwa kupelekwa shule hapo utaku umeliza kengere,”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko,amewataka waandishi wa habari kuelimisha na kukemea jamii juu ya nadharia ya dhana potofu pamoja na kuandika habari za suluhisho.

“Unawezaje kusema kidole cha mtu mwenyewe ualbino ukikikata unaweza kupata utajiri,kwanini anayekupa hayo masharti yeye ni maskini,utajiri ni sayansi hauna longolongo kama utaki kufanya kazi,utabaki kuwa maskini,”ameeleza Soko nakuongeza kuwa:

“Vyombo vya habari visiishie kuripoti tu mtu mwenyewe ualbino ameuwawa na kukutwa baadhi ya viungo vya mwili havipo ,tumechoka kusikia hivyo,zije na suluhisho kuwa licha ya mauaji yanayoendelea waje na mapendekezo ya suluhisho iwe ya kisera au utekelezaji Jeshi la Polisi lifanye nini,aidha kiushirikishwaji kwani hii vita siyo ya Jeshi la Polisi pekee,kila mwanajamii anapaswa kutambua ana nafasi ya kuzuia mauajinyaxwatu wenye ualbino,”.

Mchungaji Jacob Mutashi,amesema polisi wafanye ufuatiliaji wajue na watafute soko la wanaotafuta hivyo viungo vya watu hao na ikijulikana na soko hilo likidhibitiwa hakutakuwa na jambo hilo huku ziara za viongozi wa serikali katika mikutano yao ya hadhara ishirikishe kundi TAS,MPC,viongozi wa dini,tiba asili wale wasiopiga ramli chonganishi ili waweze kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya mapambano ya kupinga vitendo vya ukatili kwa watu wenye ualbino.

“Ndugu zangu wenye ualbino mchukue tahadhari binafsi,ulinzi binafsi ,kwani pamoja na kulindwa na serika;li kupitia jeshi la polisi msibweteke, mjue kuna hatari ,uchukue tahadahari binafsi ,tembea kama Mtanzania mwingine rudi nyumbani mapema,maeneo hatarishi,saa hatarishi ziepushe nazo,viongozi wa dini tunaenda kuliombea jambo hili,”.

Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ,SSP Dennis Kunyanja,amesema katika kuzuia na kutokomeza mauaji ya watu wenye ualbino Jeshi la Polisi kuanzia mwaka 2006 mpaka leo wanashirikisha jamii katika kuzuia uhalifu kuliko kupambana nao.

“Tukipambana kwanza namba moja yule mtu unaye mpambania tayaria ameisha uwawa unakuwa umeisha mpoteza,ndio maana nguvu kubwa tumeweka mtu wa kumlinda na kupambana na wahalifu kabla hajatenda kitendo hicho, tunaendelea na mikakati ya kuwalinda wenzetu na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza aliamua kufanya opareshi ilionza Juni 28 hadi Julai 4,2024 jumla ya watuhumiwa 63 ambao ni wapiga ramli chinganishi wamekatwa nawapo kwenye hatua mbalimbali za uchunguzi na upelelezi zikikamilika watafikishwa mahakamani,”.