December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Elimu ya PSSSF Kiganjani yawafikia wanachama maonesho ya OSHA

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umewakumbusha wanachama wake kuwa, huduma zote zinazohusiana na uanachama wa mwanachama zinapatikana mtandaoni, (PSSSF Kiganjani).

Meneja wa PSSSF, Kanda ya Kaskazini, Bi. Vonness Koka, amesema hayo wakati akiongoza timu ya watumishi wa Mfuko huo kupeleka elimu ya matumizi ya PSSSF Kiganjani kwenye mabanda ya maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), kwenye viwanja vya General Tyre jijini Arusha Aprili 25, 2025.

“Tumeanzisha mfumo wa PSSSF Kiganjani unaomuwezesha mwanachama kupata taarifa za Michango yake mahali popote alipo bila ya kufika kwenye ofisi zetu, vile vile mfumo unamuwezesha mstaafu kujihakiki akiwa nyumbani kwake, safarini au mahali popote. Tunawakaribisha wanachama wote waliopo Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Arusha na wananchi kwa ujumla, kufika kwenye banda letu ili kupata elimu hiyo ya matumizi ya PSSSF Kiganjani.” Amefafanua Bi. Koka.

Amesema, kupitia simu janja, mwanachama anachohitajika kufanya ni kupakua Application ya PSSSF Kiganjani kisha atafuata maelekezo ya namna ya kujisajili na hapo ataanza kufaidi huduma hiyo ya kisasa, amesema.

Aidha Bi. Koka amesema katika maonesho hayo pia wamekuwa wakipita kwenye mabanda na kukutana na wanachama wao lengo likiwa ni kutoa elimu hiyo ya matumizi ya PSSSF Kiganjani.

“Faida ya matumizi ya PSSSF Kiganjani, licha ya kuokoa muda, lakini pia inaondoa gharama kwa mwanachama kusafiri kufuata huduma. Pia kwa upande wa Mfuko, umepunguza gharama kwa kuachana na matumizi ya karatasi kuchapisha taarifa za wanachama wanaozihitaji.” Amesema.

Wanachama nao wameeleza faida ya huduma ya PSSSF Kiganjani.

“Nimefurahi sana kujua huduma ya PSSSF Kiganjani, lengo la kuja hapa kwenye banda la PSSSF, ni kupata taarifa za michango yangu, lakini wamenielekeza njia hii ya kutumia PSSSF Kiganjani kupitia simu yangu, nimepakua application yao na nimefanikiwa kuona taarifa zangu.” Amesema mwanachama wa PSSSF, Bw. Fabian Ndokoma.

Naye Bi. Esther Mlay, ambaye naye ni mwnaachama wa PSSF amesema yeye hana haja tena ya kwenda ofisi za PSSSF, tayari alikuwa amejiunga na PSSSF Kiganjani na amekuwa akifaidi huduma mbalimbali ikiwemo kuona mwenendo wa michango yake.

Meneja wa PSSSF, Kanda ya Kaskazini, Vonness Koka (Wanne kushoto) akiwaeleza namna ya kutumia Muongozo wa wanachama wa PSSSF, wakati yeye na timu ya watumishi wa Mfuko huo kute mbelea mambanda ya maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, kwenye viwanja vya General Tyre, Njiro, jijini Arusha Aprili 25, 2024. Lengo ni kuwapa elimu kuhusu matumizi ya PSSSF Kiganjani. Watatu kushoto ni Afisa Mkuu wa Uhusiano PSSSF, Abdul Njaidi 

Meneja wa PSSSF, Kanda ya Kaskazini, Vonness Koka (kushoto), akiwa kwenye abnda la JKCI.

Mwanachama wa PSSSF, Bw. Fabian Ndokoma

Timu ya PSSSF iliyoko maonesho ya OSHA, jijini Arusha.