Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online
MIONGONI mwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ni ukatili wa Kisaikolojia ambao una madhara kwa binadamu ye yote anapotendewa kutokana na kuathirika kiakili kutokana na kuwaza juu ya kitendo alichotendewa.
Ukatili huu unaweza kuhusiana pia na ukatili wa kiuchumi ambao athari zake zinafanana lakini mara nyingi wahanga wakuu wa ukatili wa kisaikolojia ama kiuchumi huwa ni kundi la wanawake.
Tunapozungumzia Ukatili wa Kisaikolojia tunamaanisha unaweza kutendeka kwa mtu ye yote ambaye atatendewa kitendo chenye viashiria vya udhalilishaji, kufanyiwa dhulma, kushushiwa hadhi na kunyimwa mahitaji muhimu kwa ajili ya ustawi wa familia yake.
Makala hii kwa ufupi itajikita kwenye kuangalia ukatili wanaofanyiwa wanawake wajane wengi hapa nchini baada ya kuondokewa na wanaume waliokuwa wamewaoa na hivyo kubaki wajane huku wakinyimwa haki ya kurithi mali zilizoachwa na wenza wao.
Wajane wengi pamoja na kuishi miaka mingi na waume zao hujikuta wakiangukia kwenye wimbi la umaskini baada ya kufukuzwa katika nyumba ama makazi waliyokuwa wakiishi na hali hii hujitokeza zaidi katika mkoa wa Shinyanga wanawake hawa huponzwa na sheria za kimila ambazo hazimtambui mwanamke kwenye mirathi.
Pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kutoa usawa kwa binadamu wote na haki ya kumiliki mali bila ubaguzi msingi wa jinsia, lakini bado wanawake wengi hupoteza haki hiyo baada ya kuondokewa na waume zao.
Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya Kijiji namba 5 ya mwaka 1999 zote zinatamka na kulinda haki ya kila mwanaume na mwanamke kupata, kumiliki na kudhibiti ardhi kwa masharti na vigezo sawa.
Pamoja na sheria hizo kutamka hivyo bado hapa nchini kuna vikwazo mbalimbali vinavyomzuia mwanamke asiweze kumiliki na kutumia ardhi na tukiangalia kwa umakini vikwazo hivyo huenda vinatokana na mapungufu yaliyopo katika sheria na utekelezaji wake.
Esther Medard mkazi wa kitongoji cha Mh’angu Center, kata ya Salawe Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ni mmoja wa wajane ambaye amekumbana na ukatili wa kupokonywa mali walizochuma yeye na mumewe baada ya kufariki kwa mwenza wake.
Esther anasema katika maisha yake na mumewe walikuwa wanamiliki mashamba pamoja na ng’ombe wapatao 60 na nyumba moja iliyopo kijiji cha Songambele kata ya Salawe ambapo baada ya kifo cha mumewe yeye alifukuzwa kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi.
Kibaya zaidi anasema ndugu wa marehemu mumewe (shemeji zake) ndiyo waliosimamia zoezi la yeye kufukuzwa huku akinyang’anywa baadhi ya mali ikiwemo ng’ombe wote pamoja na mashamba.
“Kwa kweli tunaiomba Serikali iangalie jinsi gani itakuwa ikiwasaidia wanawake wajane pindi wanapofiwa na waume zao na kwamba vyombo vya kutoa haki (mahakama) vijitahidi kutenda haki, ili wajane wasipoteze haki wanazostahili kuzipata katika mirathi,”
“Hawa shemeji zangu baada ya mume wangu kufariki waliungana na mke mwenzangu ambaye hakuwa mke wa ndoa wakanifukuza kwenye nyumba na kuninyan’ganya mashamba pamoja na ng’ombe wote, na amri hii ilitolewa na Baraza la ardhi la kata,” anaeleza Esther.
Esther anasema shemeji zake walifanya ujanja na kufungua kesi kwenye Baraza la Ardhi la Kata na wakashinda ambapo katika shauri hilo la mirathi walimtumia mtu asiyefahamika ndani ya familia ambaye ndiye aliyeteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi.
Anasema baada ya kushindwa kwenye Baraza la Ardhi la kata alisaidiwa kukata rufaa na baadhi ya jamaa zake na kufungua kesi kwenye Baraza la Nyumba na Ardhi ya wilaya ambako kesi ilisikilizwa na Baraza hilo la ardhi wilaya lilimpa ushindi na kuagiza arejeshewe mali zote zilizoachwa na marehemu mumewe.
“Hata hivyo hawa jamaa pamoja na kupewa ushindi na Baraza la Ardhi la wilaya, bado walikata rufaa Mahakama Kuu kitengo cha ardhi na kesi ilisikilizwa, namshukuru mungu pamoja na wao kuweka wakili kwenye kesi hii, Mahakama Kuu bado ilitupilia mbali rufaa yao na kunipa ushindi,” anaeleza Esther.
Kwa upande wake mmoja wa majirani wa Esther, Jeremiah Maganga anasema changamoto za wajane wengi kupoteza haki zao baada ya kufiwa na waume zao ni nyingi hasa katika maeneo mengi ya vijijini hali inayosababishwa na uelewa mdogo wa sheria za mirathi.
Maganga anasema Serikali ina jukumu la kuhakikisha elimu juu ya taratibu za mirathi inatolewa ili iwafikie wananchi wengi hasa walioko maeneo ya vijijini ambako mfumo dume na sheria za kimila zimetamalaki kwa kiasi kikubwa zinazochangia kwa kiasi kikubwa wanawake wajane wapoteze haki zao za mirathi.
“Kwa kweli bila juhudi za jamii kumsaidia huyu mjane, ni wazi alikuwa amepoteza haki zake zote baada ya kufiwa na mumewe, pamoja na ushindi aliopewa na Mahakama Kuu lakini tayari amejikuta akipoteza ng’ombe wote waliokuwa wa mumewe baada ya kusemekana waliisha uzwa,”
“Nafikiri umefika wakati kwa Serikali kwa sasa kutoa elimu ya kutosha kuhusiana na masuala ya mirathi na haki ambazo wanastahili kupatiwa wajane baada ya kufiwa na waume zao, hasa kwa wakazi wa vijijini, watu wengi huku vijijini bado wanatumia sheria za mila na desturi ambazo nyingi zimepitwa na wakati, sasa ni vyema elimu ya kutosha ikatolewa,” anaeleza Maganga.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Salawe wilayani Shinyanga, Emmanuel Maduhu anasema wakazi wengi wa maeneo ya vijijini bado wanatumia zaidi sheria za kimila kwenye masuala yanayohusiana na mirathi sheria ambazo kwa kiasi fulani zinaminya haki za wanawake wajane.Maduhu anasema,
“…Chini ya sheria za kimila, wajane hawana haki ya kurithi kutoka kwa waume zao kama kuna mtoto wa kiume au ndugu wa damu wa mume, sheria hizi kwa mkoa wa Shinyanga zilisimikwa mnamo mwaka 1963, ambazo kiuhalisia kwa sasa hazipaswi kufuatwa kutokana na kumnyima haki mwanamke,”Anaendelea kueleza,
“Sheria hizi humtaka mrithi wa marehemu kumtunza mjane, lakini kiuhalisia, ndugu wa marehemu mara nyingi humfukuza mjane katika makazi yake na hata kama atabaki kwenye makazi hayo bado hapewi haki ya kusimamia mali zisizohamishika.”
Kutokana na hali hiyo Maduhu pia anaunga mkono suala la Serikali hivi sasa kuendesha kampeni maalumu ya kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na suala zima la mirathi na Haki za Mwanamke kurithi mali za mumewe pindi anapokuwa amefariki.
Halima Juma mkazi wa kijiji cha Songambele kata ya Salawe wilayani Shinyanga anasema ili kuepukana na wanawake wengi wajane kutendewa vitendo vya ukatili pana kila sababu ya jamii kupewa elimu ya kutosha juu ya haki ambazo mwanamke anastahili kuzipata anapofiwa na mumewe.
“Mimi naomba Serikali ifanyie kazi suala hili, maana kwa kipindi kirefu wajane wamekuwa wakilalamika kudhulumiwa mali zao baada ya kufiwa na waume zao, hali ambayo imesababisha baadhi yao kuishi maisha ya dhiki na kufanya shughuli ndogondogo ili kuweza kujikimu kimaisha,”
“Elimu kuhusu suala la mirathi na sheria ya kumiliki ardhi namba 5 ya mwaka 1999 vikitolewa kikamilifu itasaidia kwa kiasi kikubwa wanawake kufahamu haki zao za msingi hali ambayo itanusuru wanawake wajane wengi wanaopoteza haki hizo kutokana na kutokuwa na uelewa juu ya sheria,” anaeleza Halima.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika