Na Suleiman Abeid, Timesmajira Online, Shinyanga
JANGA la maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Uviko-19 limetajwa kuendelea kusambaa katika Mataifa mbalimbali hapa duniani huku watu wengi kuambukizwa virusi vya gonjwa hilo hatari.
Mpaka hivi sasa pamoja na kwamba kasi ya maambukizi kwa hapa nchini imepungua kwa kiasi kikubwa lakini bado hali ni tete kwa vile Wizara husika ama Shirika la Afya Duniani (WHO) hawajatangaza rasmi kutoweka kwa virusi vya Uviko-19.
Ni wazi kwamba juhudi zaidi bado zinahitajika katika kukabiliana na janga hili na kuepusha maelfu ya watu kupoteza maisha yao kila kunapokucha hali inayoweza pia kusababisha kuporomoka kwa uchumi katika nchi nyingi kutokana na kupoteza nguvukazi ya watu.
Nchini Tanzania janga hili liliripotiwa kwa mara ya kwanza mnamo Machi 16, 2020 ambapo kuanzia hapo Serikali ilianza kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na gonjwa hilo lisiweze kusambaa kwa kasi zaidi pamoja na kwamba wapo baadhi ya ndugu zetu waliopoteza maisha kutokana na kupatwa na Uviko-19.
Awali Mataifa mengi ikiwemo Tanzania hayakuweza kupata dawa ya chanjo ya kukabiliana na gonjwa hili hali iliyosababisha hofu kwa wananchi wengi hasa pale taarifa za vifo vilivyotokana na Uviko 19 zilipokuwa zikitolewa.
Miongoni mwa hatua za awali zilizochukuliwa na Serikali ilikuwa ni watu kuelekezwa suala la unawaji wa mikono kwa kutumia vitakasa mikono (sanitizer) au sabuni kwa kutumia maji tiririka kila wakati hasa wanapokuwa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi.
Vilevile uvaaji wa barakoa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi ulihimizwa na viongozi wetu wa Serikali hasa katika maeneo ya maofisini, hospitali, kwenye vyombo vya usafiri na kwenye masoko, magulio na minadani.
Jitihada mbalimbali ziliendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na gonjwa hili hatari ambapo juhudi za wataalamu wa masuala ya afya duniani kote zilifanikisha kupatikana kwa dawa za chanjo kwa ajili ya kinga ya ugonjwa huu.
Kwa hapa nchini Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Julai 30, 2021 alizindua rasmi chanjo kwa ajili ya kinga ya ugonjwa wa Uviko-19 huku yeye mwenyewe akijitokeza hadharani kuchanja chanjo hiyo na akawahimiza watanzania wote wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea kujitokeza kuchanja.
Pamoja na hofu ya baadhi ya watu kuhusiana na chanjo hiyo lakini wengi wa watanzania walijitokeza na kuchanja hali ambayo inaweza kuwa moja ya sababu ya kupungua kwa maambukizi ya Uviko-19 kwa vile wengi wa waliochanjwa inakuwa vigumu kwao kuambukizwa.
Maamuzi ya Rais Samia kuruhusu chanjo hiyo yanakwenda sambamba na utekelezaji wa Sera ya Afya nchini ya mwaka 2017 ambamo ndani yake imeelezwa moja ya majukumu ya Serikali ni kuimarisha huduma za kinga na zilizo bora.
Sehemu ya Sera hiyo inaeleza, nanukuu;- “……Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na mashirika ya kimataifa itaimarisha udhibiti na uzuiaji wa magonjwa, hasa yale yanayoweza kuingizwa kutoka nje ya nchi kupitia bandarini na mipakani,” mwisho wa kunukuu.
Kutokana na Sera hii ni wazi kwamba Serikali ilikuwa na kila sababu za kuhakikisha inalinda afya za wananchi wake na ndiyo maana iliruhusu kuingizwa kwa chanjo za kinga ya Uviko-19 ili watanzania waweze kuchanja na kujikinga na ugonjwa huo ambao tayari ulikuwa umepoteza uhai wa baadhi ya watanzania wenzetu.
Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Afya hadi kufikia Novemba 04, mwaka huu jumla ya watanzania wapatao 36,362 walithibitika kuambukizwa virusi vya Uviko-19 tangu ugonjwa huo ulipoingia hapa nchini na kusababisha vifo vya watu 808 sawa na asilimia 2.22 ya waliougua tangu mlipuko huo uanze mnamo Machi, 2020.
Hata hivyo kutokana na uhamasishaji uliofanyika nchini kote kuhusu umuhimu wa chanjo kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya hadi tarehe 04 Novemba, 2022 watu waliokamilisha chanjo ya Uviko-19 tangu chanjo hiyo ilipoanza kutolewa hapa nchini walikuwa ni 26,710,881.
Mkoa wa Shinyanga pia wananchi wake wengi wamekuwa wakijitokeza kupatiwa chanjo hiyo ya kinga ya Uviko-19 pamoja na uwepo wa tafsiri potofu za baadhi ya watu kuhusiana na chanjo hiyo kudai ina madhara hivyo kusababisha baadhi ya wilaya kuwa chini kwenye utoaji wa chanjo ya Uviko-19.
Miongoni mwa Halmashauri za wilaya zilizokuwa chini hapo awali kutokana na wananchi wake kuihofia chanjo hiyo ni Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama na Kishapu mkoani Shinyanga ambapo kwa Ushetu hadi mwezi Agosti walikuwa wamechanja asilimia 59 ikiwa ni watu 106,015 huku Kishapu ikiwa na asilimia 55 sawa na watu 99,589.
Hata hivyo uhamasishaji ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya viongozi wa Serikali, Taasisi mbalimbali zisizokuwa za kiserikali na madhehebu ya dini imewezesha muamko wa baadhi ya wakazi wa mkoa wa huo hasa katika wilaya ya Kishapu ambao baada ya kuona umuhimu wake wameanza kujitokeza kuchanja chanjo hiyo.
Mratibu wa chanjo katika wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Jamila Mohamedi anasema hivi sasa kuna mafanikio makubwa upande wa uchanjaji kutokana na watu wengi kuanza kujitokeza kuchanja chanjo ya Uviko-19 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa hapo awali.
Jamila anasema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2022 wilaya ya Kishapu ilikuwa imechanja watu wapatao 123,414 kati ya walengwa 179,000 sawa na asilimia 69 ikilinganishwa na watu 99,589 waliokuwa wamechanjwa hadi kufikia mwishoni mwa Agosti, 2022 ikiwa ni asilimia 55.
Baadhi ya viongozi wa kidini wilayani Kishapu akiwemo Sheikh Adamu Njiku Sheikh wa Tarafa ya Mhunze wilayani Kishapu na Mchungaji Patrick Zengo wa kanisa la KKKT Mhunze wametoa wito kwa wakazi wa Kishapu kuendelea kujitokeza kwa wingi kuchanja chanjo hiyo kwa vile haina madhara yoyote.
Viongozi hao wamesema hakuna dini yoyote duniani inayozuia suala la chanjo na kwamba hata Mwenyezi Mungu mwenyewe anawataka waja wafanye tiba pindi wanapopatwa na magonjwa huku akihimiza suala la kulinda afya zao.
“Hata upande wetu sisi waislamu, mungu ametuagiza tunapopatwa na magonjwa tutumie dawa ili tupone, hakusema ombeni dua ili mpone, na akaagiza tujikinge na vitu vyovyote ambavyo vinaweza kutuletea madhara, ni wazi kuchanja chanjo ya Uviko-19 ni sehemu ya kujikinga,” anaeleza Sheikh Njiku.
Mchungaji Zengo mbali ya kuwapongeza watendaji wa Serikali kwa kazi kubwa ya uhamasishaji wananchi kujitokeza kuchanja chanjo hiyo pia amesema hakuna Serikali yoyote ambayo inakubali kuua wananchi wake hivyo ni wazi dawa ya chanjo ya Uviko-19 haina madhara.
“Dhana potofu ambazo zimetolewa na baadhi ya watu hapo awali ndiyo zimechangia wilaya ya yetu ya Kishapu kuwa nyuma kidogo kwa watu kujitokeza kuchanja chanjo hii ya kinga ya Uviko-19 baadhi walihisi eti mtu akichanja kisha akiwekewa balbu ya umeme inawaka, huu ulikuwa upotoshaji tu,” anaeleza mchungaji Zengo.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Maendeleo mjini Mhunze, Grace Shani anasema awali wengi walihisi wakichanjwa ndiyo wanaathirika zaidi, lakini kutokana na uhamasishaji walioufanya watu wengi wameelewa na kuona umuhimu wa kuchanja chanjo hiyo.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Mhunze wilayani Kishapu, Shabani Bakari, Asha Ramadhani na Charles Maganga wanasema awali watu wengi walishindwa kujitokeza kuchanja chanjo ya uviko-19 kutokana na hofu wakihisi chanjo hiyo ina madhara.
“Ni kweli Kishapu tulikuwa nyuma katika kuchanja chanjo hii, na hii ilichangiwa na hofu ya wengi wetu kwamba ilikuwa na madhara kwa binadamu, hasa kwa sisi watu wa jinsi ya kiume, tuliaminishwa kuwa inapunguza nguvu za kiume, kumbe siyo kweli,” anaeleza Bakari.
Mratibu wa chanjo mkoani Shinyanga, Timothy Sosoma amesema mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2022 mkoa huo umechanja watu wapatao 907,929 sawa na asilimia 90 ya lengo la kuchanja watu 1,010,085 kwa mkoa mzima wa Shinyanga hali ambayo inaonesha wengi wa wananchi wameanza kuona umuhimu wa chanjo.
Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dkt. Faustine Mlyutu anasema hadi hivi sasa mkoa wa Shinyanga uko salama kutokana na kutokuwepo mtu ye yote mwenye kesi ya virusi vya Uviko-19 na kwamba hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na mwitikio wa wananchi kujitokeza kuchanja.
“Kwa ujumla tangu tuanze kutoa chanjo hizi hatujawahi kupata maudhi yoyote yaliyojitokeza kwa wateja waliochanjwa chanjo ya kinga ya Uviko-19, na tunazidi kusisitiza kwa wakazi wote wa mkoa wetu na majirani zetu waendelee kujitokeza kuchanja chanjo hii kwa vile tayari zimeonesha matokeo chanya,” anaeleza Dkt. Mlyutu.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani