January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Elimu kuhusu athari biashara za magendo mipakani

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kutembelea mipakani kutoa elimu kuhusu biashara za magendo kwa bidhaa ambazo zinazoingia na kutoka nchini Tanzania bila kufuata taratibu za kisheria.

Maofisa wa Forodha wametembelea mpaka wa Namanga pamoja na eneo la Mundarara Longido kwa ajili ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi wanaozunguka maeneo hayo Mkoani Arusha.

Akitoa elimu hiyo Afisa Msimamizi wa Kodi Julieth Kidemi amezitaja athari za Magendo ikiwa nì kuhatarisha afya kwa watumiaji wa bidhaa zilizoingia kwa Magendo bila kupitia maeneo yaliyo ainishwa na Serikali kwajili ya ukaguzi na kupimwa kama zinafaa kwa matumizi ya binadamu.

Aidha ameongeza kuwa athari nyingine ya Magendo nì uingizwaji wa vifaa ambavyo vinaweza kuwa na athari kwa usalama wa nchi ikiwemo mabomu na bunduki, hivyo kuhatarisha usalama wa Nchi.

Sambamba na hayo amewatahadharisha kuacha kufanya biashara za magendo kwani kufanya hivyo kutasababisha kushuka kwa uchumi wa Nchi.

Pia alieleza adhabu za kisheria zitakazo chukuliwa kwa atakaye kamatwa na mzigo wa Magendo ambapo adhabu hizo ni pamoja na kifungo na faini.

Ametoa wito kwa wananchi hao kutumia mipaka rasmi ambayo imeweka na Serikali katika uingizaji na utoaji wa mizigo, lengo likiwa ni kuthibitisha ubora wa bidhaa hizo kutoka mamlaka husika zilizopo.

“Serikali inapowataka wananchi wapite kwenye mipaka rasmi sio kwa ajili ya kodi peke yake, maana kuna bidhaa nyingine hazilipiwi kodi, ila wanataka kwa ajili ya kupata takwimu Ili kujua kilichoingia na kutoka nchini “Amesema Afisa Kidemi.

Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa forodha Mkoa wa Arusha, Bw. Paul Kamukulu ameshukuru kwa ujio wa Maafisa kutoka kitengo cha elimu kwenda kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi wanaokaa maeneo ya mipakani kuhusiana umuhimu wa kupita mipaka iliyo rasmi, hivyo kwa elimu hiyo itawasaidia wananchi kuacha kuingiza bidhaa za magendo na kufata taratibu zilizowekwa na Serikali.

Nao wafanyabiashara waliopata Semina hiyo wameishukuru TRA, huku wakiomba Serikali kupunguza makali ya sheria za mipakani ili waweze kufanya biashara zao bila vizuizi.