Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKURUGENZI wa Taasisi ya Msaada wa Kisheria ya Everlasting Legal Aid Foundation (ELAF), Dkt. Khamis Masoud, ameiomba serikali kutunga sheria mpya ya Judicial Transparency and Digital Access Act itakayowezesha kuanzishwa kwa mahakama za kidijitali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Dkt. Masoud amesema sheria hiyo itarahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi, kuongeza uwazi wa mashauri mahakamani, na kutoa fursa ya elimu ya sheria kwa njia ya kidijitali.
“Tunahitaji mfumo wa kisasa wa mahakama ambao utamwezesha kila mwananchi, hata akiwa kijijini, kufuatilia mashauri yenye maslahi mapana kwa nchi kupitia njia za mtandao,” Amesema Dkt. Masoud.
Amebainisha kuwa mahakama za kidijitali zitasaidia kupunguza gharama, kuongeza usalama, na kurahisisha ujifunzaji wa sheria kwa vitendo.
Aidha, ametoa mfano wa kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa Tundu A. Lissu ambapo wananchi walizuiwa kuingia mahakamani kwa madai ya ukosefu wa nafasi na sababu za kiusalama.
“Kuwazuia wananchi kushuhudia mashauri kama haya ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 13(6)(a), pamoja na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu, ibara ya 7,” amefafanua
Dkt. Masoud alipendekeza mahakama zote nchini kuwa na mfumo wa matangazo ya moja kwa moja (livestreaming) kupitia YouTube na tovuti rasmi, pamoja na kuanzishwa kwa Idara Maalum ya Mahakama ya Kidijitali chini ya Ofisi ya Jaji Mkuu.
Aidha, alishauri kuanzishwa kwa vituo vya ufikiaji wa huduma za mahakama kwa jamii (Court Access Hubs) katika ofisi za kata au vituo vya msaada wa kisheria, ili kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika mfumo wa utoaji haki.
“Falsafa ya ‘mahakama ya wazi’ haipaswi kumaanisha tu milango wazi, bali pia taratibu, mwenendo na matokeo ya mashauri yote yawe wazi na kufuatiliwa kwa njia mbalimbali, ikiwemo kidijitali,” amesema.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa bajeti mahsusi ya TEHAMA kwa ajili ya mahakama na kushirikisha wananchi katika hatua zote za utekelezaji wa mabadiliko hayo ya kidijitali.
Katika hatua nyingine, Dkt. Masoud alitoa wito kwa Watanzania kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 kwa amani na utulivu, huku akihimiza kuepuka vitendo vya fujo vinavyoweza kuwaletea madhara kisheria.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina